Upload
phungnhu
View
326
Download
0
Embed Size (px)
Citation preview
i
MUHTASARI
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ilifanya utafiti kwa lengo la kutoa ushauri
sahihi juu ya njia na namna ya kuziba mianya ya rushwa katika huduma zinazotolewa na Hospitali ya
Mkoa wa Morogoro. Aidha, utafiti ulikuwa na madhumuni yafuatayo: (a) kubaini mianya ya rushwa
katika mlolongo wa utoaji huduma; (b) kubaini na kuainisha vikwazo vya utoaji huduma; (c)
kupendekeza namna bora ya kuziba mianya ya rushwa; na (d) kudhibiti kutorudiwa kwa mbinu na
taratibu zinazoonekana kuwa ni vyanzo vya rushwa. Ukusanyaji wa taarifa ulifanyika kwa kipindi cha
majuma mawili kuanzia tarehe 02 Oktoba hadi 16 Oktoba 2010.
Utafiti huu ulitokana na ombi rasmi la Ofisi ya Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro na uongozi wa
Hospitali, kutokana na kutambua athari mbaya za rushwa katika maboresho ya Hospitali ya Mkoa wa
Morogoro na wajibu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kisheria. Hospitali
ya Mkoa wa Morogoro ipo kwenye maboresho makubwa ya huduma na miundombinu ya Hospitali.
Maboresho ya huduma yanahusu upatikanaji wa dawa muhimu, vifaa na vitendea kazi. Aidha, maboresho
ya miundombinu yanahusu ujenzi wa majengo mapya, ukarabati wa majengo ya zamani, kuboresha
Teknolojia ya Mawasiliano na Habari (ICT), na kuboresha mfumo wa umeme, maji safi na maji taka.
Kwa upande wa fedha, Hospitali inalenga kuongeza mapato yake kupitia uchangiaji. Hospitali hiyo
inakabiliwa na malalamiko ya wateja kuhusu vitendo vya rushwa dhidi ya watumishi wake.
Mbinu zilizotumika katika ukusanyaji wa taarifa zilihusisha: taarifa za msingi (primary data), taarifa za
upili (secondary data) na Utambuzi wa Mtafiti (Non-Participant Observation). Taarifa za msingi
zilitokana na mahojiano rasmi kwa njia ya madodoso, mjadala (kikao na Menejimenti ya Hospitali) na
mahojiano yasiyo rasmi. Taarifa za upili zilipatikana kwenye sera, sheria, miongozo ya utendaji kazi na
nyaraka nyingine muhimu. Kuhusu utambuzi wa mtafiti, watafiti walihusika na kuangalia mazingira ya
kazi, vitendea kazi, utendaji kazi, na mwenendo wa wadau.
Matokeo ya utafiti yanabainisha mianya ya rushwa katika makundi matatu: uwajibikaji mdogo wa
watumishi, uwazi mdogo wa huduma na upungufu wa maadili. Uwajibikaji mdogo unasababishwa na
udhaifu wa udhibiti wa ndani hasa katika unaibishaji, mawasiliano ya ndani, mbinu za uongozi, tathmini
za utendaji, ufanyaji maamuzi, na udhibiti wa rasilimaliwatu. Uwazi mdogo wa huduma za Hospitali
umesababisha mambo yafuatayo: kutojulikana kwa haki za wagonjwa; kutojulikana kwa taratibu za
huduma; kutojulikana na kutoimarika kwa Kitengo cha kupokelea na kushughulikia malalamiko; na
kuwepo kwa mawasiliano duni kati ya Hospitali na wadau. Upungufu wa maadili, pamoja na mambo
ii
mengine, umesababishwa na ufahamu mdogo wa rushwa na madhara yake, na maana na namna ya
kukabiliana na mtanziko wa maadili.
Aidha, upungufu wa maadili umesababisha mahusiano mabovu kati ya wagonjwa na watumishi ambayo
yanasababishwa na lugha mbaya ya watumishi kwa wagonjwa, wizi wa dawa walizopewa wagonjwa, na
watumishi kutovaa vitambulisho na kutia ugumu wa kutambuliwa na wagonjwa. Vilevile, upungufu wa
maadili unasababishwa na kutokuwepo au udhaifu wa vyombo vinavyosimamia maadili (yaani Kamati ya
Nidhamu na kamati ya Maadili). Aidha, wahojiwa walitoa maoni yaliyoonyesha kuwa sehemu ya
upasuaji inaongoza kwa rushwa ikifuatiwa na mapokezi na wodi ya wazazi.
Utafiti uliainisha mbinu za kudhibiti rushwa katika Hospitali ya Mkoa wa Morogoro kuwa ni kuboresha
maslahi, kuhakikisha utoshelevu wa rasilimali, elimu ya maadili kwa watumishi, mafunzo kazini, na
kuimarisha uwazi na uwajibikaji.
iii
YALIYOMO
MUHTASARI ................................................................................................................................................ i
YALIYOMO ................................................................................................................................................ iii
Orodha ya majedwali ................................................................................................................................... iv
Orodha ya Viambatanisho ............................................................................................................................. v
Orodha ya vifupisho ..................................................................................................................................... vi
1. UTANGULIZI ..................................................................................................................................... 1
2. MATOKEO YA UTAFITI ................................................................................................................... 2
2.1 Vikwazo vya utendaji katika hospitali ...................................................................................... 2
2.2 Uwajibikaji hospitalini .............................................................................................................. 4
2.3 Uwazi wa huduma katika hospitali ........................................................................................... 8
2.4 Vitendo vya Rushwa hospitalini ............................................................................................... 9
2.5 Maoni ya wahojiwa ................................................................................................................. 10
3. MAPENDEKEZO .............................................................................................................................. 12
3.1.1 Mapendekezo kwa hospitali ................................................................................................ 12
4. MKAKATI WA KUDHIBITI MIANYA YA RUSHWA ................................................................. 15
5. HITIMISHO ....................................................................................................................................... 18
iv
Orodha ya majedwali
Jedwali 1: Maoni ya wahojiwa kuhusu maeneo ya hospitali yanayohitaji udhibiti wa rushwa
Jedwali 2: Maoni ya wahojiwa kuhusu mbinu za kudhibiti rushwa hospitalini
Jedwali 3: Mapendekezo kwa hospitali ya mkoa wa Morogoro
Jedwali 4: Mkakati wa kuboresha huduma Hospitali ya mkoa wa Morogoro
v
Orodha ya Viambatanisho
Kiambatanisho I: Muundo wa Hospitali ya Mkoa wa Morogoro
Kiambatanisho II: Thamani ya vifaa na dawa-Hospitali ya Mkoa wa Morogoro 2009/10
Kiambatanisho III: Makusanyo na matumizi ya fedha za uchangiaji huduma za afya 2009/10
vi
Orodha ya vifupisho
HMT - Hospital Management Team
ICT - Information and Communication Technology
IPD - In-Patient Department
KRAs - Key Result Areas
MKUKUTA
MOI/C
- Mkakati wa Kuondoa Umasikini na Kukuza Uchumi
Medical Officer Incharge
MSD - Medical Stores Department
OPD - Out Patient Department
OPRAS - Open Performance Review and Appraisal System
RAS
RHMT
-
Regional Administrative Secretary
Regional Health Management Team
TAKUKURU - Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
TUGHE - Trade Union for Government Health Employee
1
1. UTANGULIZI
Mapambano dhidi ya rushwa katika sekta ya afya ni muhimu katika kufanikisha mpango wa maboresho
wa sekta hiyo unaotekelezwa na serikali. Mpango huo unalenga kuziwezesha Hospitali za Mikoa kuwa za
rufaa ili kuongeza ubora wa huduma kwa maana ya kupanua upatikanaji wake, na kuongeza dawa na
watumishi wenye sifa katika ngazi ya mkoa. Maboresho haya yanafanyika kwa kuzingatia Sera ya Taifa
ya Afya ya mwaka 2003 inayohimiza, pamoja na mambo mengine, kuongeza usambazaji wa dawa na
vifaa ili kukidhi mahitaji ya vituo vya afya (health facilities) na kutoa mafunzo kazini kwa watumishi
ambao utendaji wao wa kazi hauridhishi kutokana na kukosa mafunzo ya kutosha.
Hospitali ya Mkoa wa Morogoro ipo kwenye maboresho makubwa ya huduma na miundombinu ya
Hospitali. Maboresho ya huduma yanahusu upatikanaji wa dawa muhimu, vifaa na vitendea kazi. Aidha,
maboresho ya miundombinu yanahusu ujenzi wa majengo mapya, ukarabati wa majengo ya zamani,
kuboresha Teknolojia ya Mawasiliano na Habari (ICT), na kuboresha mfumo wa umeme, maji safi na
maji taka. Kwa upande wa fedha, Hospitali inalenga kuongeza mapato yake kupitia uchangiaji. Hospitali
inakabiliwa na msongamano wa wagonjwa kwa sababu kuu mbili: moja, inategemewa kwa rufaa na
wilaya zote tano za mkoa wa Morogoro. Mbili, hutumiwa kila siku na wilaya za Morogoro na Mvomero
kwa kuwa katika wilaya hizo hakuna hospitali za wilaya. Vilevile, Hospitali inakabiliwa na malalamiko
ya wateja kuhusu vitendo vya rushwa dhidi ya watumishi wake.
Kwa kutambua athari za rushwa katika maboresho ya Hospitali na wajibu wa Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kisheria, Ofisi ya Katibu Tawala Mkoa na uongozi wa Hospitali
waliiomba TAKUKURU kufanya utafiti kwa lengo la kutoa ushauri sahihi juu ya njia na namna ya kuziba
mianya ya rushwa katika huduma zinazotolewa na Hospitali ya Mkoa wa Morogoro. Aidha, utafiti
ulikuwa na madhumuni yafuatayo: (a) kubaini mianya ya rushwa katika mlolongo wa utoaji huduma; (b)
kubaini na kuainisha vikwazo vya utoaji huduma; (c) kupendekeza namna bora ya kuziba mianya ya
rushwa; na (d) kudhibiti kutorudiwa kwa mbinu na taratibu zinazoonekana kuwa ni vyanzo vya rushwa.
2
2. MATOKEO YA UTAFITI
Matokeo ya utafiti yanaonesha kuwepo vikwazo vya kimuundo na kiutendaji, uwajibikaji na
uwazi mdogo wa huduma, na vitendo vya rushwa katika Hospitali hiyo ya Mkoa kama ifuatavyo:
2.1 Vikwazo vya Utendaji Katika Hospitali
a) Vikwazo vya kimuundo na kiutendaji katika Hospitali ya Mkoa wa Morogoro
Matokeo yanaonyesha kuwepo vikwazo vya kimuundo na kiutendaji katika Hospitali ya Mkoa wa
Morogoro. Kwa wastani wahojiwa walieleza kuwepo udhibiti mdogo wa uwajibikaji (43%), mawasiliano
duni kati ya viongozi na wafanyakazi (53%), mawasiliano duni kati ya idara (40%), mawasiliano duni
baina ya Hospitali na wadau wengine (43%), mishahara midogo (30%), na upungufu wa vitendea kazi
(21%) na wafanyakazi (11%). Upungufu wa vitendea kazi unatajwa kuwa, pamoja na mambo mengine,
unatokana na ubora mdogo wa vifaa vinavyotolewa na MSD. Vifaa vya MSD vinadaiwa kuwa havidumu
muda mrefu kwa kuwa aghalabu havitimizi hata mwaka mmoja baada ya kuanza kutumika.
Aidha, matokeo yanabainisha kuwa kikwazo kikubwa ni mawasiliano duni kati ya uongozi na
wafanyakazi na baina ya Hospitali na wadau wengine, haya yamejipambanua zaidi kwa wauguzi na
watumishi wengine. Hata hivyo, TUGHE wao wameeleza kuwa wana ushirikiano mzuri na menejimenti
ya Hospitali. Mawasiliano duni yanasababisha kutokuwepo maelewano kati ya wafanyakazi na uongozi
na hivyo kusababisha wafanyakazi kukata tamaa na kujihusisha na vitendo kinyume na maadili ya
utumishi wa umma. Vilevile, mwanya mwingine unatokana na Hospitali kutokuwa na Bodi ya Hospitali
(Kiambatanisho I) na hivyo kukwaza ushiriki wa jamii katika usimamizi wa Hospitali. Kwa mfano,
kutokana na umuhimu wa Bodi katika kudhibiti ukusanyaji na kuidhinisha matumizi ya mapato ya
Hospitali, kutokuwepo kwake kunasababisha majukumu ya Bodi kufanywa na Kamati ya Uendeshaji ya
Hospitali au Mganga Mfawidhi wa Hospitali.
Hali hii inaonesha kuwa kazi za utendaji na usimamizi zinafanywa na mtu yuleyule (ukiritimba –
monopoly) na hivyo kutoa mwanya wa wafanyakazi kujihusisha na vitendo vinavyokwenda kinyume na
taratibu na sheria zinazoongoza huduma za afya. Kwa upande wa unaibishaji mamlaka (delegation),
umebainika udhaifu wa baadhi ya watumishi kuingiliwa kazi zao na walio juu yao, na hatimaye kuathiri
mlolongo wa uwajibikaji (accountability chain) katika Hospitali. Kamati ya Uendeshaji ya Hospitali ya
Mkoa (RHMT) inatajwa kuingilia kazi za utendaji za Kamati ya Uendeshaji ya Hospitali (HMT)
kiutawala (administratively), kifedha (financially) na kitaaluma (technically). Hali hii inatajwa kuwa
inatokana na viongozi na watumishi kukosa mbinu za uongozi (managerial skills) na kutokuwa na
3
maelezo ya kazi zao (job description). Muundo unawapa watumishi nafasi za uongozi wa Hospitali kwa
taaluma zao (technical skills), lakini wanakosa mbinu za uongozi. Hivyo, ili kuondoa muingiliano wa kazi
na kuongeza uwajibikaji, watumishi wa Hospitali wanapaswa kuwa na maelezo ya kazi zao na pia
kupatiwa mafunzo ya mbinu za uongozi.
Kwa upande wake tofauti ya kimtazamo kati ya viongozi, madaktari na wauguzi kuhusu uchache wa
watumishi kuwa chanzo cha rushwa, inaonesha haja ya kufanyika mjadala zaidi katika hili. Tofauti na
viongozi, wauguzi na madaktari, watumishi wengine wote walieleza kuwa uchache wa watumishi si
kikwazo cha utendaji. Hali hii inaweza kuelezeka kuwa huenda kundi hili likawa na sababu nyingine zaidi
ya hii ambazo kwao ndiyo kikwazo cha utendaji. Lakini kwa mujibu wa matokeo, watumishi wengine
wanaona kuwa udhibiti mdogo wa uwajibikaji na mawasiliano duni baina ya Hospitali na wadau kuwa
ndiyo vikwazo vya utendaji.
Jitihada za kudhibiti vikwazo hivyo zinatajwa kufanyika katika Hospitali, lakini ni wastani wa asilimia 38
tu ya wahojiwa ambao walieleza kuwepo jitihada za kuimarishwa kwa mawasiliano baina ya Hospitali na
wadau wengine. Matokeo yanaonesha kusigana kwa makundi mbalimbali ya watumishi kuhusu jitihada
zinazofanywa kudhibiti vikwazo vilivyobainika. Viongozi, takribani wote, wanaeleza kuwepo kwa
jitihada za kudhibiti vikwazo, kinyume na maoni ya watumishi waliobaki ambao wengi hawaoni kama
jitihada zinafanywa kukabili vikwazo hivyo. Kusigana kwa makundi haya ya watumishi kunaashiria
kuwepo mkwamo wa utiririkaji wa taarifa kimuundo kutoka juu kwenda chini. Hatua madhubuti na za
makusudi zinapaswa kufanywa ili kuondoa vikwazo na kuboresha mtiririko wa taarifa (information flow).
b) Uwepo wa Mkataba wa Huduma kwa Mteja na Kamati ya Kudhibiti Maadili
Matokeo yanaonyesha kuwa Hospitali ya Mkoa wa Morogoro bado haijatayarisha Mkataba wa Huduma
kwa Mteja, na vilevile haijaunda Kamati ya Kudhibiti Maadili Hospitalini hapo (hii ni kwa mujibu wa
kikao cha Menejimenti cha tarehe 02/10/2010). Ukweli huu unakinzana na majibu ya wahojiwa wengi
ambao wanaeleza kuwepo kwa Kamati ya maadili (70%) na Mkataba wa Huduma kwa Mteja (52%).
Wahojiwa hawa wanashindwa kutofautisha kati ya Kamati ya Maadili na Kamati ya Nidhamu, na kati ya
Mkataba wa Huduma kwa Mteja na miongozo na matangazo mbalimbali ya Hospitali yanayoelekeza
kuhusu huduma kwa wagonjwa. Mkanganyiko huo unaimarisha dhana kuwa uongozi na watumishi wengi
wa Hospitali hawaifahamu miongozo muhimu ya kitaifa ya kudhibiti maadili na kuongeza uwajibikaji wa
watumishi. Kutofahamu huko kunatoa mwanya mkubwa wa vitendo vya rushwa na mkengeuko wa
maadili.
4
c) Muda ambao mtumishi amefanya kazi katika Hospitali ya mkoa wa Morogoro
Matokeo yanaonesha kuwa, kwa wastani, asilimia 46 ya watumishi waliohojiwa wamekwishakaa kwenye
eneo moja la kazi kwa muda unaozidi miaka mitano, wengi wao wakiwa ni wauguzi na watumishi
wengine. Hali hii inatoa mwanya mkubwa wa vitendo vya rushwa na ukiukwaji wa maadili kwa
watumishi hasa wauguzi ambao wamekuwa wakilalamikiwa kwa vitendo hivyo.
2.2 Uwajibikaji Hospitalini
a) Jinsi uwajibikaji wa watumishi wa Hospitali unavyopimwa
Matokeo ya utafiti yanaonesha kuwa wastani wa asilimia 67 ya wahojiwa walieleza kuwa utendaji
hospitalini hapo hupimwa kwa Utaratibu wa Wazi wa Tathmini za Utendaji (Open Performance Review
and Appraisal System – OPRAS). Hata hivyo, baadhi ya wahojiwa wakiwemo TUGHE wanaeleza kuwa
OPRAS haijaanza kwa kuwa upimaji bado unafanywa kwa siri kupitia miundo ya utumishi - ‘scheme of
service’. Aidha, wastani wa asilimia 52 ya wahojiwa walieleza kuwa uwajibikaji unapimwa kwa
kuzingatia uandishi wa taarifa za uwajibikaji zenye kuzingatia maadili ya kitaalamu na viwango bora vya
utendaji na zenye kuonesha kilichofanyika, kilichotumika na kwa nini. Hata hivyo, wahojiwa wachache
(wastani wa asilimia 34 tu) walieleza kuwa upimaji wa uwajibikaji katika Hospitali ya Mkoa wa
Morogoro hufanywa kwa kuzingatia matumizi bora ya rasilimali.
Matokeo haya yanabainisha tashwishi ya kutokuwepo udhibiti imara wa uwajibikaji hasa kwa kuzingatia
kuwa ni nusu tu ya viongozi waliohojiwa ambao walieleza kuwepo kwa uandishi wa taarifa za uwajibikaji
na matumizi sahihi ya rasilimali. Viongozi wote waliohojiwa walieleza kuwa OPRAS inatumika kupima
uwajibikaji kinyume na maelezo ya makundi mengine ya watumishi yaliyohojiwa. Hali hiyo huenda
inasababishwa na OPRAS kuwa ndiyo kwanza imeanza kutumika katika mwaka huu wa fedha wa
2010/11 Hospitalini hapo na inawezekana kuwa watumishi bado hawajaelimishwa vya kutosha kuhusu
lengo na faida za OPRAS.
Mbinu nyingine inayoweza kudhibiti uwajibikaji ni kukagua mahudhurio ya watumishi na kuchukua
hatua zifaazo kwa wachelewaji, watoro na wasiohudhuria kazini. Matokeo ya ukaguzi wa daftari la
mahudhurio yanaonesha kuwa daftari hilo hukaguliwa kila siku, lakini halina sehemu kwa ajili ya kusaini
watumishi wanaokwenda nje ya Hospitali ndani ya muda wa kazi. Kwa upande wa wachelewaji kazini,
uongozi unaeleza kuwa wachelewaji hujadiliwa katika vitengo vyao na wanapozidi wanapelekwa kwenye
Kamati ya Nidhamu ya Hospitali. Aidha, kumbukumbu za vikao vya Kamati ya Uendeshaji ya Hospitali
zinaonesha kuwa suala la utoro limekuwa likijadiliwa mara kwa mara.
5
b) Uwepo wa kitengo cha kupokelea na kushughulikia malalamiko ya wagonjwa katika hospitali
Matokeo yanaonesha kuwa wastani wa asilimia 54 ya wahojiwa walieleza kuwepo kwa Kitengo cha
Kupokelea na Kushughulikia Malalamiko Hospitalini hapo. Hata hivyo, muhtasari wa kikao cha Kamati
ya Uendeshaji ya Hospitali cha tarehe 02/08/2010 na mahojiano na baadhi ya viongozi yanabainisha kuwa
kitengo hicho hakikuwa na ofisi na kwamba uongozi ulikuwa katika maandalizi ya ofisi na kuajiri afisa
mwenye taaluma ya ustawi wa jamii kwa ajili hiyo. Aidha, Hospitali inayo masanduku ya maoni ambayo
kwa idadi, kama yalivyohesabiwa na watafiti, masanduku hayo hayazidi kumi, na kuna baadhi ya wodi
masanduku hayo hayapo. Kwa mujibu wa maelezo ya wahojiwa na kuthibitishwa na kumbukumbu za
vikao vya HMT, inaonekana kuwa malalamiko yanapokelewa kupitia masanduku au taarifa ya moja kwa
moja kwenye ofisi ya Mganga Mfawidhi wa Hospitali na hatimaye kwenye Kamati ya Nidhamu ya
Hospitali. Masanduku ya Maoni hufunguliwa na Sekretarieti ya Mkoa (Afisa Utumishi wa Mkoa) kila
baada ya miezi mitatu (3). Utafiti ulipitia mihtasari ya vikao vya HMT na kubaini kuwepo mashauri ya
nidhamu ya baadhi ya watumishi wa Hospitali. Hata hivyo, baadhi ya wahojiwa walieleza kuwa kamati
haichukui hatua zipasazo kutokana na woga walionao wajumbe wa kamati hiyo.
Vilevile, matokeo yanaonesha kuwa Kitengo cha Kupokelea na Kushughulikia malalamiko hakifahamiki
kwa watumishi wengine wengi (56%), na wagonjwa wa ndani wote (100%) na wagonjwa wa nje wote
(100%). Hali hii inatokana na kutowekwa wazi kwa kitengo hicho muhimu. Uwazi huu mdogo
unasababishwa na kutokuwepo kwa mbao za matangazo za kutosha na kutokuwepo kwa bango
linalowaelekeza wagonjwa kuhusu kutoa maoni au malalamiko yao kwenye kitengo hicho. Hali hii
inaashiria kuwepo udhaifu katika Hospitali wa kushughulikia malalamiko ya wagonjwa hasa ikizingatiwa
kuwa baadhi ya Wakuu wa Idara (22%) walieleza kutokuwepo Kitengo cha Kupokelea na Kushughulikia
Malalamiko.
Kuhusu namna ambavyo malalamiko yanapokelewa Hospitalini hapo, wastani wa asilimia 74 ya
wahojiwa walieleza kuwa malalamiko yanapokelewa kwa njia ya sunduku la maoni. Njia nyingine za
kupokelea malalamiko zilitajwa kuwa ni ofisi ya kitengo cha malalamiko (63%), vyombo vya habari
(17%), viongozi wa Hospitali (16%) na kuwahoji wagonjwa baada ya hatua yao ya mwisho ya huduma
(Exit Interview) (4%).
Hata hivyo, maelezo ya kupokelewa malalamiko kupitia ofisi ya Kitengo cha Kupokelea Malalamiko,
yanakosa mashiko kwa kuwa Kitengo hicho hakikuwa na ofisi Hospitalini hapo. Vilevile, ilifahamika
kwenye kikao na Menejimenti ya Hospitali cha tarehe 02/10/2010 kuwa pamekuwepo na utaratibu wa
kuwahoji wateja wanapoondoka hospitalini baada ya kupata huduma (Exit Interview); kwa lengo la
kutathmini utendaji na kufahamu malalamiko na maoni ya wagonjwa, lakini matokeo ya utafiti huu
6
yanaonesha kuwa Madaktari, wauguzi na watumishi wengine hawafahamu kama ‘Exit Interview’
hutumika kukusanyia malalamiko ya wagonjwa. Muhtasari wa kikao cha Kamati ya Uendeshaji ya Mkoa
na Kamati ya Uendeshaji ya Hospitali cha tarehe 14/07/2010 unatoa taarifa ya matokeo ya ‘Exit
Interview’ iliyofanyika hospitalini hapo na hivyo kuonesha kuwa inafanyika, hali inayoashiria kuwa
huenda taarifa sahihi kuhusu kinachojiri kwenye vikao hivyo huwa haziwafikii watumishi wengi.
c) Muda ambao mgonjwa umetumia kupata huduma
Matokeo yanaonesha kuwa wastani wa asilimia 71 ya wahojiwa walieleza kusubiri muda mrefu (masaa
mawili hadi matano) kabla ya kumwona daktari na aghalabu hucheleweshewa majibu ya vipimo.
Aidha, wamezitaja huduma zinazotolewa kwa muda wa chini ya masaa mawili kuwa ni kumwona daktari
(73%) na x-ray (54%). Huduma ambayo imeelezwa kutumia muda mrefu ni kupata majibu ya maabara.
Uchelewaji wa majibu ya maabara (saa 2 na zaidi) umetajwa na nusu ya wagonjwa wa nje kuliko
wagonjwa wa ndani (19%), hali ambayo huenda inatokana na wagonjwa wa ndani kutohusika moja kwa
moja na ufuatiliaji wa vipimo vyao. Aidha, hali hii inaweza kuwa inatokana na uchache wa madaktari na
watumishi wa maabara, na upungufu wa vifaa.
Hata hivyo, kwa ujumla wastani wa asilimia 28 ya wahojiwa walieleza kuwa muda wa huduma ulikuwa
bora, wakati asilimia 36 ya wahojiwa walieleza kuwa muda wa huduma Hospitalini hapo haufai.
Matokeo haya yanatofautiana na matokeo ya ‘Exit Interview’ yaliyotolewa kwenye Kikao cha
RHMT/HMT cha tarehe 14/07/2010 ambapo ilibainishwa kuwa asilimia 80 (wagonjwa 16 kati ya 20) ya
wagonjwa waliridhika na huduma za Hospitali. Hali hii inaonesha umuhimu wa kufanya tathmini za mara
kwa mara kuhusu kuridhika kwa wagonjwa juu ya huduma za Hospitali, badala ya kuegemea kwenye
tathmini moja tu.
d) Vikwazo ambavyo mgonjwa amepata wakati wa kupata huduma
Matokeo yanaonesha kuwa wastani wa asilimia 38 ya wahojiwa, hasa wagonjwa wa nje, walieleza
kuwahi kukwazwa na madaktari na wauguzi wakati wa huduma katika Hospitali ya Mkoa wa Morogoro.
Aidha, wastani wa asilimia 56 ya waliokwazwa, hasa wagonjwa wa ndani, waliwahi kukaripiwa na
wauguzi wa Hospitali ya Mkoa wa Morogoro. Kuwepo kwa lugha mbaya katika Hospitali
kunadhihirishwa pia na azimio la wajumbe wa kikao cha RHMT/HMT cha tarehe 14/07/2010 la kutaka
jitihada zifanyike kuondoa lugha mbaya ya watumishi.
7
Kwa upande wa wagonjwa kupewa nafasi ya kujieleza, asilimia 33 ya wagonjwa wa ndani walieleza
kutopewa muda wa kujieleza na daktari. Vilevile, wastani wa asilimia 62 ya wagonjwa walieleza
kutopatiwa dawa zote walizoandikiwa na daktari kutokana na upungufu wa dawa ikilinganishwa na
mahitaji. Kumbukumbu za Hospitali zinaonesha kuwa thamani ya dawa na vifaa kwa mwaka wa fedha wa
2009/10 ilikuwa ni shilingi 156,367,021.18 (Kiambatanisho II) ambazo utolewaji wake haukufanywa
kwa wakati na kusababisha Hospitali kukabiliwa na madeni. Aidha, kuna tatizo la udhibiti mdogo wa
fedha za Hospitali zinazopelekwa MSD kwa kuwa Hospitali haijulishwi na Wizara ya Afya kuhusu
mgawo huo. Vilevile, tatizo la wizi wa dawa za wagonjwa nalo linapunguza upatikanaji wake; mara
nyingine baadhi ya watumishi wa Hospitali walilalamikiwa kuwa walichukua dawa za wagonjwa wa
ndani kwa manufaa yao. Hata hivyo, katika maelezo yao wagonjwa wote waliohojiwa walieleza kuwa
hawajawahi kupeleka malalamiko yao kwa uongozi wa Hospitali.
Matokeo haya yanaashiria uwezekano wa kufanyika vitendo vya rushwa kutokana na hofu inayojengwa
kwa mgonjwa kiasi cha mgonjwa kushindwa kuomba usaidizi au kuhoji mambo anayofanyiwa kinyume
na haki zake kama mgonjwa. Hali inaweza kupelekea baadhi ya wagonjwa au ndugu/jamaa wa wagonjwa
kutumia pesa kama nyenzo ya kupunguza ukali wa wauguzi. Vilevile, hali hii inaweza kupunguza ufanisi
wa utendaji katika Hospitali. Ukali wa watoa huduma unaweza pia kuwakimbiza wagonjwa kutoka
Hospitali ya Mkoa wa Morogoro na kwenda kutafuta huduma kwingine na hata kwenye tiba za kienyeji,
na hivyo kukwaza jitihada za serikali za kuhakikisha wananchi wake wote wanapata huduma bora za
afya.
e) Mgonjwa kupatiwa stakabadhi kwa malipo ya huduma aliyoyafanya
Matokeo ya dodoso kwa wagonjwa yanaonesha kuwa wastani wa asilimia 52 ya wagonjwa walikuwa
wamelipia huduma, wengi wao ni wagonjwa wa nje (79%), wastani wa asilimia 90 ya wagonjwa
waliolipia huduma walipatiwa stakabadhi kwa malipo waliyoyafanya. Hata hivyo, wastani wa asilimia 10
ya wagonjwa walieleza kutopatiwa stakabadhi kwa malipo waliyoyafanya ambapo baadhi walieleza
kutolipia huduma kwa kuwa walikuwa kwenye utaratibu wa msamaha.
Wagonjwa waliohojiwa wanaeleza kuwa walifahamu gharama za huduma kupitia mbao za matangazo
(24%), kuelezwa mapokezi (37%), na kwa kuelezwa na daktari (33%).
Hospitali imeweka wazi na kuheshimu utaratibu wa kutoa msamaha kwa wagonjwa kwa maana ya
kuhakikisha ujazwaji sahihi wa fomu maalumu ya msamaha na vibali kwa wagonjwa wa ndani na wa nje.
Hata hivyo, Hospitali bado haina Afisa Ustawi wa Jamii ambaye ni mtu muhimu sana katika usimamizi
wa misamaha. Kwa upande wa wagonjwa wa ndani, hasa nyakati za usiku, Muuguzi Mfawidhi wa zamu
8
ndiye anayeidhinisha msamaha wa muda kwa wagonjwa wenye sifa za kupewa msamaha. Uidhinishaji
wa msamaha katika Hospitali ya Mkoa wa Morogoro inafanywa na Mganga Mfawidhi. Kwa upande wa
baadhi ya wagonjwa kutopewa stakabadhi, kunaashiria pamoja na mambo mengine, uwezekano wa
kuwepo upotevu wa mapato ya Hospitali yatokanayo na uchangiaji wa gharama za matibabu. Kwa mfano
katika mwaka wa fedha 2009/10 Hospitali ililenga kukusanya shilingi 200,000,000.00 lakini ikakusanya
shilingi 134,468,418.00 (67%) (Kiambatanisho III). Sababu nyingine zinazotajwa kupunguza mapato ni
mpangilio mbaya wa majengo ya Hospitali kwa ajili ya wagonjwa wa nje (OPD) na wagonjwa wa ndani
(IPD), rushwa na upendeleo katika misamaha. Muhtasari wa kikao cha HMT cha tarehe 16/07/2010
unabainisha kuwa misamaha ya wagonjwa ina harufu ya rushwa kutokana na shinikizo za watumishi wa
ngazi mbalimbali wa Hospitali kutaka watu wao wapewe misamaha. Aidha, kikao cha HMT cha tarehe
02/08/2010 kilionesha kutoridhishwa na ukusanyaji wa mapato na kuwataka watumishi wote kuwajibika
ipasavyo.
Kuhusu mpangilio wa OPD na IPD, Hospitali kihistoria ilikuwa ni kambi ya jeshi, hivyo haina mpangilio
wa kihospitali kiasi cha OPD na IPD kutojipambanua vyema. Hali hii inarahisisha kutoroka kwa
wagonjwa wanaopewa msamaha wa muda – yaani msamaha unaolazimisha kulipia huduma zinazofuata.
Kwa hali ilivyo sasa katika Hospitali, ni vigumu kumdhibiti mgonjwa iwapo ataamua kutoroka.
2.3 Uwazi wa Huduma katika Hospitali
a) Wagonjwa kufahamu haki zako wakati wa kupata huduma na njia waliyotumia kuzifahamu
Matokeo yanaonesha kuwa wastani wa asilimia 48 tu ya wagonjwa ndiyo walikuwa wanafahamu haki
zao; wengi wao (52%) walikuwa hawazifahamu haki zao hasa wagonjwa wa ndani (69%).
Aidha, wagonjwa walieleza kuzifahamu haki zao kupitia kuelezwa na wafanyakazi wa Hospitali (20%),
mbao za matangazo za Hospitali (30%), kuelezwa na jirani (41%), na vyombo vya habari (57%).
Haki ambazo wagonjwa wengi walieleza kuzifahamu ni pamoja na: haki ya kuhudumiwa kwa muda
sahihi (94%), haki ya kusikilizwa (90%), haki ya kutotamkiwa lugha ya ukali (79%), na haki ya
kujulishwa taratibu za huduma (53%).
Ufahamu mdogo wa wagonjwa kuhusu haki zao ni mwanya wa rushwa hasa kwa wagonjwa wa ndani
ambao pia walieleza kuchukuliwa dawa zao na watumishi wa Hospitali. Huenda kutofahamu haki kwao
huko ndiko kulikosababisha wao kuchelea kutoa taarifa za vitendo vya wizi wa dawa zao. Vilevile,
matokeo yanaashiria kuwa huenda wagonjwa wengi hawasomi mbao za matangazo za Hospitali na hivyo
kuwepo haja ya kubuni utaratibu mzuri wa kuwaelekeza wagonjwa na kuwapa elimu wananchi na
9
wagonjwa kuhusu haki na wajibu wao katika huduma za afya. Kwa kuanzia Hospitali inapaswa
kutekeleza utaratibu uliotajwa katika kikao cha HMT cha tarehe 02/08/2010 kuhusu kuwepo mtu maalum
wa kuwaelekeza wagonjwa (mfano; mtu aliyevaa nguo iliyoandikwa “NIULIZE MIMI”).
b) Uwazi katika mlolongo wa huduma
Taratibu za huduma za Hospitali zinapaswa kuwa wazi kwa wagonjwa ili kudhibiti mianya ya rushwa na
hatimaye kuongeza ufanisi wa utoaji huduma. Matokeo yanaonesha kuwa wastani wa asilimia 61 ya
wagonjwa walieleza kuwa mlolongo wa kupata huduma umewekwa wazi.
Hata hivyo, kuwepo kwa idadi kubwa ya wagonjwa wa ndani (63%), kwa maana ya jumla ya walioeleza
kutowekwa wazi kwa mlolongo wa huduma (19%) na wasiojua kama mlolongo wa huduma upo wazi
(44%), kunaashiria kuwa taratibu za huduma kwa wagonjwa wa ndani hazifahamiki kwa wagonjwa.
Kutofahamika huko kunatoa mwanya wa vitendo vya rushwa katika wodi za Hospitali.
2.4 Vitendo vya Rushwa Hospitalini
a) Wagonjwa walioshuhudia vitendo vyovyote vinavyoashiria rushwa Hospitalini
Matokeo yanaonesha kuwa wastani wa asilimia 38 ya wagonjwa walishuhudia vitendo vinavyoashiria
rushwa kutendeka Hospitalini hapo. Walivitaja vitendo vinavyoashiria rushwa kuwa ni: mgonjwa kupata
kitanda wakati wodi imefurika, mgonjwa kuombwa fedha ya soda na wauguzi, upendeleo kwa baadhi ya
wagonjwa, na kutopewa risiti ya malipo.
Kwa upande wao, watafiti wanakubaliana na maelezo ya wagonjwa ya kuwepo vitendo vya rushwa
Hospitalini hapo kwa sababu zifuatazo: Kwanza, mahojiano na viongozi yanadhihirisha kupokelewa kwa
malalamiko kumi (10) ya rushwa dhidi ya watumishi wa Hospitali katika kipindi cha kuanzia mwishoni
mwa 2009 hadi Oktoba 2010. Pili, waliokataa kushuhudia vitendo vya rushwa, walifanya hivyo kutokana
na woga waliokuwa nao wakati wa mahojiano. Wastani wa asilimia 62 ya wagonjwa waliokataa
kushuhudia vitendo vya rushwa, wengi wao wakiwa ni wagonjwa wa ndani (67%) walionekana kuwa na
hofu, kwa kuangalia maeneo mbalimbali ya wodi, pale walipoulizwa swali la kama wameshuhudia
vitendo vinavyoashiria rushwa. Hofu ya wagonjwa ilionekana kuzidi pale wauguzi walipopita karibu yao
wakati wa mahojiano. Hali hiyo ilimfanya mgonjwa mmoja kusita kujibu kwa sauti na badala yake
kuendelea kuitikia kwa ishara ya kichwa. Hofu yao inatia shaka ya kama walichokuwa wanaeleza ndicho
walichomaanisha. Hofu hiyo, ilisababisha wengi wao kudai kusikia zaidi kuliko kushuhudia moja kwa
moja na hivyo kukwepa ingawa si moja kwa moja. Hofu na woga wa wananchi umekuwa unakwaza
jitihada za serikali za kupambana na rushwa nchini Tanzania.
10
Sababu nyingine ya wagonjwa kukwepa kueleza kama walishuhudia vitendo vya rushwa inaweza
kutokana na kuogopa kuwa mashahidi dhidi ya watumishi husika hasa katika utambuzi wa watumishi
husika. Woga huu unaweza kuwa unachangiwa na baadhi ya watumishi kutokuwa na vitambulisho vya
kuvaa, na hata walionavyo, vitambulisho vyao havifanani kwa ubora kwa watumishi wote kiasi cha
kuwachanganya wagonjwa. Hali hii inakwaza utoaji wa malalamiko ya rushwa dhidi ya watumishi kwa
kuwa inakuwa vigumu kumtambua mtumishi husika.
b) Mafunzo ya utawala bora na mapambano dhidi ya rushwa kwa watumishi
Matokeo yanaonesha kuwa wastani wa asilimia 56 ya wahojiwa walieleza kupatiwa mafunzo ya utawala
bora na mapambano dhidi ya rushwa. Hata hivyo, madaktari wengi (78%), watumishi wengine (44%),
wauguzi (25%) na Wakuu wa Idara (22%) hawajapata mafunzo ya utawala bora na mapambano dhidi ya
rushwa ikilinganishwa na Menejimenti ambao wote walieleza kupatiwa mafunzo hayo. Matokeo haya
yanarandana na uadilifu mdogo wa baadhi ya watumishi waliotajwa kwenye kikao cha HMT cha tarehe
30/09/2010. Vilevile, Mpango Mkakati wa Hospitali wa 2009/10 hauzungumzii mapambano dhidi ya
rushwa katika ‘Key Result Areas’ (KRAs) zote hasa ‘KRA1’ inayohusika na rasilimaliwatu, ingawa zana
zilizotumika kama mwongozo wa kuweka vipaumbele vya kukabiliana na matatizo ya afya ya msingi
zinatajwa kuwa ni pamoja na MKUKUTA na Malengo ya Maendeleo ya Milenia. Mojawapo ya malengo
ya MKUKUTA ni kujenga utawala bora yakiwamo mapambano dhidi ya rushwa. Hali hii inaashiria
uwezekano wa ukiukwaji wa maadili kwa makundi hayo ya watumishi wa Hospitali ya Mkoa wa
Morogoro, hasa kwa kuzingatia kuwa Hospitali haijaunda Kamati ya Maadili.
2.5 Maoni ya Wahojiwa
Katika kutafuta mbinu za kudhibiti mianya ya rushwa katika Hospitali ya Mkoa wa Morogoro,
watumishi wa Hospitali, wagonjwa, CSOs na TUGHE waliombwa kuainisha sehemu za Hospitali
zenye rushwa na namna ya kuidhibiti Hospitalini hapo. Maoni ya wahojiwa yanaonesha kuwa sehemu
ya upasuaji inaongoza kwa rushwa ikifuatiwa na mapokezi na wodi ya wazazi (jedwali 1).
11
Jedwali 1; Maoni ya wahojiwa kuhusu maeneo ya Hospitali yanayohitaji udhibiti wa
rushwa
Eneo Alama
(%)
Upasuaji 21.6
Mapokezi 20.3
Wazazi (Labour) 14.9
Uhasibu 13.5
Maabara 12.2
Manunuzi 9.4
Utawala 8.1
JUMLA 100.0
Vilevile, waliainisha mbinu za kudhibiti rushwa katika Hospitali ya Mkoa wa Morogoro kuwa ni
kuboresha maslahi, kuhakikisha utoshelevu wa rasilimali, elimu ya maadili kwa watumishi, mafunzo
kazini, na kuimarisha uwazi na uwajibikaji. Uboreshaji wa maslahi ya watumishi umepata alama za juu,
ukifauatiwa na elimu ya maadili na rushwa kwa watumishi wa Hospitali na kusimamia uwajibikaji
(Jedwali 2).
Jedwali 2; Maoni ya wahojiwa kuhusu mbinu za kudhibiti rushwa Hospitalini
Mbinu Alama
(%)
Kuboresha maslahi ya watumishi 15.5
Kutoa elimu kwa watumishi kuhusu maadili na rushwa 14.7
Kusimamia uwajibikaji 13.2
Kuongeza na kuboresha vitendea kazi 11.6
Kuchukua hatua dhidi ya wala rushwa 10.8
Kutoa elimu kwa wananchi kuhusu taratibu za huduma 8.5
Kuongeza watumishi 5.4
Kuhakikisha uwiano mzuri wa mafunzo kwa watumishi 4.6
Kuondoa matabaka na upendeleo sehemu ya kazi 3.1
Kujenga hospitali za wilaya 3.1
Kuchunguza stakabadhi 3.1
Nyingine (kuongeza uwazi katika idara, kutoa fedha kulingana na bajeti, watumishi
wasikae eneo moja muda mrefu, na kuanzisha rejesta ya wagonjwa wa upasuaji)
6.4
JUMLA 100.0
12
3. MAPENDEKEZO
3.1.1 Mapendekezo kwa hospitali
Jedwali 3: Mapendekezo kwa Hospitali ya Mkoa wa Morogoro
Na. MIANYA YA
RUSHWA
MAPENDEKEZO YA KUZIBA MIANYA YA RUSHWA
1.0 UWAJIBIKAJI
MDOGO WA
WATUMISHI
WA
HOSPITALI
1.1 Kuboresha udhibiti wa ndani kwa kuzingatia yafuatayo:
Kuzingatia matakwa ya muundo ya unaibishaji wa mamlaka (yaani
majukumu na maamuzi);
Kuweka wazi mlolongo wa uwajibikaji;
Kuimarisha mawasiliano ya ndani;
Kuwapatia watumishi maelezo ya kazi zao (job description);
Kuwepo, kutambulika na kutumika kwa Mkataba wa Huduma kwa
Mteja;
Kufanywa kwa tathmini za utendaji (OPRAS na Exit Interview);na
Kufanya ukaguzi wa kushtukiza mara kwa mara; na uwazi katika
maamuzi kwa kuzingatia sheria.
1.2 Kuondoa ucheleweshaji wa huduma kwa kufanya yafuatayo:
Kusimamia mahudhurio na kudhibiti utoro wa watumishi;
Kuhamisha watumishi waliokaa sehemu moja ya kazi kwa muda
mrefu; na
Kufanya kazi kulingana na sheria, kanuni na taratibu.
1.3 Kuongeza tija ya watumishi kwa kufanya yafuatayo:
Kuboresha maslahi, mishahara na motisha kwa watumishi;
Kudhibiti manunuzi na usambazaji wa dawa na vifaa unaofanywa na
MSD;
Kuimarisha usimamizi wa rasilimaliwatu, dawa, na vifaa-tiba;
Kusimamia mapato na matumizi ya fedha; na
Kulipa stahili za watumishi ipasavyo.
13
2.0 UWAZI
MDOGO WA
HUDUMA
1.1 Kuimarisha mawasiliano ya Hospitali na wadau.
1.2 Kuweka wazi HAKI za WAGONJWA na taratibu za huduma kwa wadau
wote kwa njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na vipeperushi na vyombo vya
habari.
1.3 Kukiimarisha na kukiweka wazi Kitengo cha Kupokelea na
Kushughulikia Malalamiko kwa maana ya:
Kuongeza masanduku ya maoni;
Kuwa na vhumba kinachokidhi kupokea malalamiko;
Kuwepo watumishi maalum wa Kitengo;
Kukitangaza kitengo cha kushughulikia malalamiko kwa wadau;
Kuwepo Kamati Maalum ya kufungua masanduku ya maoni na
kupitia maoni. Aidha, mihtasari ya vikao vya kamati iwe inaandikwa;
na
Masanduku ya Maoni yafunguliwe kila baada ya wiki 2.
1.4 Kuimarisha mawasiliano ya Hospitali na wadau.
3.0 UPUNGUFU
WA MAADILI
3.1 Kuongeza ufahamu wa watumishi na wananchi kuhusu rushwa kwa
kufanya yafuatayo:
Kutoa elimu ya mtanziko wa maadili (ethical dilemma) na jinsi ya
kukabiliana nao;
Kutoa elimu ya huduma bora kwa mteja;
Mafunzo kwa watumishi kuhusu suala la maadili;
Kutilia mkazo elimu ya madhara ya rushwa; na
Kuuingiza mkakati wa Hospitali wa kupambana na rushwa katika
Mpango Mkakati wa mwaka wa Hospitali.
3.2 Kuboresha mahusiano kazini kati ya mgonjwa/mdau na mtumishi kwa
kufanya yafuatayo:
Kuondoa lugha mbaya na wizi wa dawa za wagonjwa; na
Kuwapatia watumishi wote vitambulisho vya kuvaa.
3.3 Kuendeleza maadili, nidhamu na uwajibikaji wa watumishi kwa kufanya
yafuatayo:
Kuboresha Kamati ya Nidhamu kwa kuzingatia matakwa ya Sheria ya
Mahusiano ya Kazi ya mwaka 2004;
Kuundwa, kutambulika na kufanya kazi kwa Kamati ya Maadili;
Kuweka wazi majukumu ya Kamati ya Nidhamu, na makosa, adhabu
14
na haki ya kukata rufaa;
Kutoa zawadi kwa watendaji bora na kuwaadabisha wakosaji;
Kuimarisha usimamizi wa misamaha ya wagonjwa;
Kuondoa aina yoyote ya ubaguzi kazini; na
Kulipa stahili za watumishi.
3.1.2 Mapendekezo Kwa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inashauriwa kuboresha uwajibikaji wa watumishi wa Sekta ya Afya
nchini kwa kufanya yafuatayo:
(i) Madaktari waliopewa madaraka wapatiwe mafunzo ya Uongozi na Utawala. Chuo cha Utumishi wa
Umma kinaweza kuendesha mafunzo hayo (TAKUKURU inaweza kusaidia);
(ii) Kusimamia uundwaji wa Bodi za Hospitali nchini;
(iii) Kujenga Hospitali za Wilaya za Morogoro na Mvomero;
(iv) Kuendelea na uboreshaji wa miundombinu ili kutenganisha OPD na IPD; na
(v) Kuongeza tija ya watumishi kwa kufanya yafuatayo:
Kuongeza mishahara na motisha kwa watumishi;
Kudhibiti manunuzi na usambazaji wa dawa na vifaa unaofanywa na MSD; na
Kuongeza watumishi na vifaa.
15
4. MKAKATI WA KUDHIBITI MIANYA YA RUSHWA
Baada ya kukamilika utafiti, TAKUKURU kwa kushirikiana na uongozi wa Mkoa na Hospitali ya
Morogoro iliandaa warsha ya kujadili matokeo. Warsha hii ilifanyika tarehe 10 Desemba, 2010 mjini
Morogoro na kuweka maazimio ya utekelezaji katika kudhibiti mianya ya rushwa iliyobainika katika
utafiti. Baada kuweka maazimio washiriki waliweka mkakati wa kudhibiti mianya ya rushwa ili
kuboresha huduma katika Hospitali ya Mkoa wa Mororgoro (Jedwali 4).
Jedwali 4: Mkakati wa Kuboresha Huduma za Hospitali ya Mkoa Morogoro.
Na
.
MAPUNGUFU
/MIANYA YA
RUSHWA
MAAZIMIO/MAPENDEKEZO
1.0 Uwajibikaji
mdogo wa
watumishi wa
Hospitali.
Kuboresha udhibiti wa ndani kwa kuzingatia yafuatayo:-
Kuzingatia matakwa ya muundo ya unaibishaji wa mamlaka (yaani
majukumu na maamuzi),
Kuweka wazi mlolongo wa uwajibikaji
Kuimarisha mawasiliano ya ndani
Kuwapatia watumishi maelezo ya kazi zao (job description)
Kuwepo, kutambulika na kutumikak wa Mkataba wa Huduma kwa
Mteja
Kufanywa kwa tathmini za utendaji (OPRAS na Exit Interview)
Kufanya ukaguzi wa kushtukiza mara kwa mara, na uwazi katika
maamuzi kwa kuzingatia sheria.
Kuondoa ucheleweshaji wahuduma kwa kufanya yafuatayo:-
- Kusimamia mahudhurio na kudhibiti utoro wa watumishi na
Kuhamisha watumishi waliokaa sehemu moja ya kazi kwa muda
mrefu.
Kufanya kazi kulingana na sheria, kanuni na taratibu
Kuongeza tija ya watumishi kwa kufanya yafuatayo:
- Kuboresha maslahi, mishahara na motisha kwa watumishi.
Kudhibiti manunuzi na usambazaji wa dawa na vifaa unaofanywa na
MSD.
16
Kuimarisha usimamizi wa rasilimali watu, dawa, na vifaa-tiba; na
Kusimamia mapato na matumizi ya fedha.
Kulipa stahili za watumishi ipasavyo
2.0 Uwazi mdogo
wa Huduma
Kuimarisha mawasiliano ya Hospitali na wadau
Kuweka wazi HAKI za WAGONJWA na taratibu za huduma kwa
wadau woe kwa njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na vipeperushi na
vyombo vya habari
Kukiimarisha na kukiweka wazi Kitengo cha kupokelea na
kushughulikia malalamiko kwa maana ya:-
- Kuongeza masanduku ya maoni
Kuwa na chumba kinachokidhi kupokea malalamiko
Kuwepo watumishi maalum wa kitengo
Kukitangaza kitengo cha kushughulikia malalamiko kwa wadau
Kuwepo Kamati Maalum ya kufungua masanduku ya maoni na
kupitia maoni. Aidha, mihtasari ya vikao vya Kamati iwe
inaandikwa.
Masanduku ya maoni yafunguliwe kila baada ya wiki 2
3.0 Upungufu wa
maadili
Kuongeza ufahamu wa watumishi na wananchi kuhusu rushwa kwa
kufanya yafuatayo:-
- Kutoa elimu ya mtanziko wa maadili (Ethical dilemma) na jinsi
ya kukabiliana nao.
Kutoa elimu ya huduma bora kwa mteja
Mafunzo kwa watumishi kuhusu suala la maadili.
Kutilia mkazi elimu ya madhara ya rushwa, na kuingiza mkakati wa
Hospitali wa kupambana na rushwa katika Mpango Mkakati wa
mwaka wa Hospitali.
Kuboresha mahusiano kazini kati ya mgonjwa/mdau na mtumishi
kwa kufanya yafuatayo:-
- Kuondoa lugha mbaya na wizi wa dawa za wagonjwa
Kuwapatia watumishi wote vitambulisho vya kuvaa
Kuendeleza maadili, nidhamu na uwajibikaji wa watumishi kwa
kufanya yafuatayo:-
- Kuboresha Kamati ya Nidhamu kwa kuzingatia matakwa ya
17
Sheria ya Mahusiano ya Kazi ya mwaka 2004.
Kuundwa, kutambulika na kufanya kazi kwa Kamati ya Maadili.
Kuweka wazi majukumu ya Kamati ya Nidhamu, na makosa ,
adhabu na haki ya kukata rufaa.
Kutoa zawadi kwa watendaji bora na kuwaadabisha wakosaji.
Kuondoa aina yoyote ya ubaguzi kazini
4.0 Mapendekezo
kwa Wizara ya
Afya na Ustawi
wa jamii
Madaktari waliopewa madaraka wapatiwe mafunzo ya Uongozi na
Utawala, Chuo cha Utumishi wa Umma kinaweza kuendesha
mafunzo hayo. Aidha, TAKUKURU inaweza kusaidia.
Kusimamia uundwaji wa Bodi za Hospitali nchini
Kujenga Hospitali za halmashauri ya Wilaya za Manispaa,
Morogoro na Mvomero
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii waendelee kusapoti
utenganishaji wa OPD na IPD
Kuongeza tija ya watumishi kwa kufanya yafuatayo:-
- Kuongeza mishahara na motisha kwa watumishi
- Kudhibiti manunuzi na usambazaji wa dwa na vifaa unaofanywa
na MSD, na
- Kuongeza watumishi na vifaa
18
5. HITIMISHO
Mianya ya rushwa iliyobainika katika huduma za Hospitali ya Mkoa wa Morogoro imeainishwa katika
makundi matatu ambayo ni: uwajibikaji mdogo wa watumishi, uwazi mdogo wa huduma za Hospitali, na
upungufu wa maadili.
Uwajibikaji mdogo unasababishwa na udhaifu wa udhibiti wa ndani hasa katika unaibishaji, mawasiliano
ya ndani, mbinu za uongozi, tathmini za utendaji, ufanyaji maamuzi, na udhibiti wa rasilimaliwatu.
Uwazi mdogo wa huduma za Hospitali umesababisha mambo yafuatayo: kutojulikana kwa haki za
wagonjwa; kutojulikana kwa taratibu za huduma; kutojulikana na kutoimarika kwa Kitengo cha
Kupokelea na Kushughulikia Malalamiko; na kuwepo kwa mawasiliano duni kati ya Hospitali na wadau.
Upungufu wa maadili pamoja na mambo mengine umesababishwa na ufahamu mdogo wa rushwa na
madhara yake, na maana na namna ya kukabiliana na mtanziko wa maadili. Aidha, upungufu wa maadili
umesababisha mahusiano mabovu kati ya wagonjwa na watumishi ambayo yanasababishwa na lugha
mbaya ya watumishi kwa wagonjwa, wizi wa dawa walizopewa wagonjwa, na watumishi kutovaa
vitambulisho na kutia ugumu wa kutambuliwa na wagonjwa. Vilevile, upungufu wa maadili
unasababishwa na kutokuwepo au udhaifu wa vyombo vinavyosimamia maadili (yaani Kamati ya
Nidhamu na kamati ya Maadili). Kamati ya Nidhamu iliyopo imelalamikiwa kuwa ni dhaifu kutokana na
kutochukua hatua zifaazo dhidi ya wakosaji. Udumavu wa kamati hiyo unatajwa kuwa unasababishwa na
woga wa wanakamati, na kutowekwa wazi kwa: kanuni zinazoongoza kazi za kamati; majukumu ya
kamati; makosa; adhabu; na haki ya kukata rufaa. Hata hivyo, Hospitali haina Kamati ya Maadili na hivyo
kusababisha mwanya wa ukiukwaji wa maadili. Utafiti unaamini kuwa iwapo serikali na uongozi wa
hospitali utayatafutia ufumbuzi mambo haya kama ambavyo imependekezwa, vitendo vya rushwa
vitadhibitiwa na huduma itaboreka zaidi hospitalini hapo.
19
VIAMBATANISHO
Kiambatanisho I: Organization Structure of Morogoro Regional Hospital
RDO RR RHET RLT RNO
HAB RMCHC
C
MOI/C
HHS HMT
HEAD PARTMENTS NOI/C HO OS
NO
ET ANAE STHE
T IST
PAEDIA
TRICIAN PATHO
LOGIST
SURG
EON
PHYSI
CIAN OBSGYN
PHAR
MACI ST
PHYS IOTH
MED.
SOC. W CASUALITY
AND OPD
OFFICER
OPTHAL
MOLOGIST DENTAL
OFFICER
RADIO
LOGIST
RMO
RPHCC
RHMT RHS
RE RHO RO
OCC
THER
ORTH
TECH
20
RMO – Regional Medical Officer RPHCC – Regional Primary Health Care
Coordinator/Committee
RHS – Regional Health Secretary RHMT – Regional Health Management Team
RNO – Regional Nursing Officer RMCH-CO – Regional Maternal & Child Health Coordinator
RE – Regional Epidemiologist RHO – Regional Health Officer
RP – Regional Pharmacist RO – Regional Ophthalmologist
RR – Regional Radiographer RDO – Regional Dental Officer
RLT – Regional Laboratory Tech. RHET – Regional Hospital Engineering Technician
HAB – Hospital Advisory Board MOI/C – Medical Officer In charge
HHS – Hospital Health Secretary HMT – Hospital Management Team
NOI/C – Nursing Officer In charge HO – Health Officer
OS – Office Supervisor ET – Engineering Technician
OBSGYN – Obstetrician &
Gynecologist
MED.SOC.W – Medical Social Worker
PHYSIOTH - Physiotherapist OCC.THER – Occupational Therapist
ORTH-TECH – Orthopaedic
Technician
CHANZO:Hospitali ya Mkoa wa Morogoro
Kiambatanisho II: Thamani ya vifaa na dawa-Hospitali ya Mkoa wa Morogoro 2009/10
TAREHE FEDHA
17/07/2009 27,364,018.09
08/09/2009 8,630,759.25
14/10/2009 16,312,739.10
14/10/2009 9,272,898.00
18/12/2009 15,188,558.00
17/03/2010 16,078,336.56
17/03/2010 5,383,061.40
10/05/2010 9,493,835.70
25/05/2010 3,432,000.00
15/06/2010 34,167,620.89
15/06/2010 7,531,194.19
JUMLA 156,367,021.18
CHANZO:Hospitali ya Mkoa wa Morogoro
21
Kiambatanisho III: Makusanyo na matumizi ya fedha za uchangiaji huduma za afya 2009/10
MWEZI MAKUSANYO MATUMIZI
Agosti……………………………………………………. 10,525,600/= 7,647,105/=
Septemba………………………………………………… 12,631,600/= 14,306,458/=
Oktoba……………………………………………………. 9,533,200/= 13,226,780/=
Novemba………………………………………………… 8,649,200/= 11,611,250/=
Desemba…………………………………………………. 14,517,200/= 8,088,400/=
Januari……………………………………………………. 13,831,600/= 8,293,361/=
Februari…………………………………………………… 12,191,200/= 5,798,200/=
Machi……………………………………………………… 12,653,618/= 15,154,200/=
Aprili……………………………………………………… 12,688,900/= 16,012,630/=
Mei………………………………………………………… 13,875,100/= 11,288,600/=
Juni………………………………………………………… 13,371,200/= 9,153,000/=
JUMLA 134,468,418/= 120,579,984/=
CHANZO:Hospitali ya Mkoa wa Morogoro