8/13/2019 Hotuba Ya Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Mhe Joseph S. Warioba, Ripoti ya Tume kwa Rais Kikwet
1/23
1
HOTUBA YA MWENYEKITI WA TUME YA MABADILIKO YA
KATIBA, MHE. JOSEPH S. WARIOBA WAKATI WA KUKABIDHI
RIPOTI YA TUME KWA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA
TANZANIA, MHE. DKT. JAKAYA MRISHO KIKWETE NARAIS WA ZANZIBAR MHE. DKT. ALI MOHAMED SHEIN;
TAREHE 30 DESEMBA, 2013, DAR ES SALAAM
________________
Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Dkt. Mohamed Gharib Bilal, Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar naMwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi;
Mheshimiwa Mizengo Kayanza Peter Pinda, Waziri Mkuu;
Mheshimiwa Maalim Seif Sharif Hamad, Makamu wa Kwanza waRais wa Zanzibar;
Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi, Makamu wa Pili wa Rais waZanzibar;
Mheshimiwa Anne Makinda, Spika wa Bunge la Jamhuri yaMuungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Pandu Ameir Kificho, Spika wa Baraza laWawakilishi;
Mheshimiwa Mohamed Chande Othman, Jaji Mkuu wa Tanzania;
Mheshimiwa Omar Othman Makungu, Jaji Mkuu wa Zanzibar;
Mheshimiwa Mzee Ali Hassan Mwinyi, Rais wa Pili wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania;
8/13/2019 Hotuba Ya Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Mhe Joseph S. Warioba, Ripoti ya Tume kwa Rais Kikwet
2/23
2
Mheshimiwa Mzee Benjamin Mkapa, Rais wa Tatu wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania;
Waheshimiwa Viongozi wote mliopo hapa;
Waheshimiwa Mabalozi;
Ndugu wananchi;
Mheshimiwa Rais,
Kwa makubaliano na Mheshimiwa Rais wa Zanzibar, tarehe 6 Aprili,
2012 ulituteua kuwa wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba,
ulituapisha tarehe 13 Aprili na tulianza kazi tarehe 2 mei, 2012. Tulikuwa
34, yaani wajumbe 32 na Katibu na Naibu Katibu. Leo tuko hapa 32.
Kama inavyofahamika tulimpoteza mjumbe mmoja, Dr. Sengondo Mvungi
katika mazingira ya kusikitisha.Mungu aiweke roho yake mahali pema
peponi. Mjumbe mwingine, ndugu John Nkolo, hayuko hapa kutokana na
matatizo ya kiafya. Hali yake inaendelea vizuri. Vile vile mjumbe wa
sekretariati ndugu Onorius Njole aliugua wakati Tume ilipokuwa
inasimamia Mabaraza ya Katiba. Naye pia hali yake inaendelea vizuri.
Mheshimiwa Rais,
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ilitoa miezi kumi na nane kwa Tume
kukamilisha kazi yake. Sheria pia ilitoa nafasi ya Tume kuongezewa
muda usiozidi miezi miwili na Tume iliomba muda huo na ulitukubalia.
8/13/2019 Hotuba Ya Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Mhe Joseph S. Warioba, Ripoti ya Tume kwa Rais Kikwet
3/23
3
Kazi tuliyopewa tumeikamilisha na leo tupo tayari kukabidhi kwako
na kwa Mheshimiwa Rais wa Zanzibar Ripoti yetu kama sheria
inavyoelekeza. Ripoti tunayoikabidhi inaambatana na taarifa saba
zifuatazo:-
(i) Maoni ya Wananchi kuhusu Mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri yaMuungano wa Tanzania;
(ii) Maoni ya Mabaraza ya Katiba kuhusu Rasimu ya Katiba ya Jamhuriya Muungano wa Tanzania;
(iii) Maoni ya Wananchi kuhusu Sera, Sheria na Utekelezaji;(iv) Takwimu za Ukusanyaji wa maoni ya Wananchi kuhusu Mabadiliko
ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
(v) Utafiti kuhusu Mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano waTanzania;
(vi) Viambatisho vya Ripoti ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba; na(vii) Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Rais,
Kabla ya kukabidhi Ripoti yetu naomba univumilie niweze kusema
machache lakini kwa maneno mengi. Napenda kuanza na shukrani. Baada
ya kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kukamilisha kazi hii,
shukrani zetu kwanza ni kwako Mheshimiwa Rais na Mheshimiwa Rais wa
8/13/2019 Hotuba Ya Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Mhe Joseph S. Warioba, Ripoti ya Tume kwa Rais Kikwet
4/23
4
Zanzibar. Tunawashukuru kwa kututeua na pia kwa msaada mkubwa
mliotupa. Kila tulipokwama mahali mlikuwa wepesi kutoa maagizo
yaliyotukwamua. Tunawashukuru sana Mawaziri wa Katiba na Sheria,
Wanasheria Wakuu wa Serikali, Makatibu Wakuu Viongozi na Watendaji
Wakuu wa Wizara za Katiba na Sheria, Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa
Wilaya, Wakurungenzi na Makatibu wa Mamlaka za Serikali za Mitaa,
Watendaji wa Tarafa, Kata na Shehia, Vijiji na Wenyeviti wa Serikali za
vijiji kwa ushirikiano mzuri walioutoa kwa Tume. Aidha, Tume inatoa
shukrani za dhati kwa Jeshi la Polisi na Kamati za Ulinzi na Usalama za
Wilaya kwa kuhakikisha mchakato mzima unakamilika kwa usalama.
Tume pia inatoa shukrani kwa Vyama vya siasa, Jumuiya za Dini,
Asasi za Kiraia, Taasisi na makundi mengine kwa mchango wao. Kwa
namna ya pekee, tunavishukuru vyombo vya habari ambavyo, licha ya
kusambaza taarifa mbalimbali zilizokuwa zikitolewa na Tume,
vimeuelimisha Umma na kuufanya mchakato mzima wa katibakuwa wa
wazi na wenye hamasa.
Mwisho kwa uzito wa pekee Tume inawashukuru wananchi, hasa
wananchi wa kawaida, kwa mchango wao mkubwa wa mawazo na maoni.
Hii ni mara ya kwanza katika nchi yetu kwa wananchi wa kawaida
kushiriki katika kutoa maoni kuhusu aina ya Katiba wanayoitaka na
wamefanya hivyo kwa wingi na kwa uzito mkubwa.
8/13/2019 Hotuba Ya Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Mhe Joseph S. Warioba, Ripoti ya Tume kwa Rais Kikwet
5/23
5
Mheshimiwa Rais,
Kama nilivyosema mapema, pamoja na Ripoti ya Tume kuhusu
mchakato wa katiba ambayo tunakabidhi leo, tunakabidhi pia na Rasimu
ya Katiba. Rasimu hiyo ni ndefu kuliko Rasimu ya awali. Rasimu ya awali
ilikuwa na ibara 240. Rasimu ya sasa ina ibara 271. Ongezeko la ibara
kwa kiwango kikubwa limetokana na Tume kuzingatia maoni ya Mabaraza
ya Katiba. Muhtasari wa Rasimu uko kwenye Sura ya Kumi na Mbili ya
Ripoti yetu. Kwa leo nitagusia mambo machache ambayo Tume imeona
vyema tukatoa maelezo.
Jambo la kwanza, ni ushiriki wa wananchi katika mchakato mzima
wa kupata katiba mpya. Tume ilipoanza kulikuwa na wasiwasi kwamba
ushiriki wa wananchi wa kawaida ungekuwa dhaifu kwa sababu iliaminika
kwamba wananchi kwa ujumla wao hawana ujuzi wa katiba. Lakini Tume
iligundua mapema kwamba wananchi wanajua mambo mengi ambayo ni
msingi wa katiba yoyote ile.
Sura tano za mwanzo za Rasimu ya Katiba zinatokana na mchango
mkubwa kutoka kwa wananchi, hasa kuhusu Misingi ya Taifa, Tunu za
Taifa, Maadili na Miiko ya Uongozi, Dira ya Taifa na Haki za binaadam.
Wananchi pia wametoa maoni mazito kuhusu uongozi na utawala wa
nchi, ikiwa ni pamoja na nafasi ya wawakilishi wao Bungeni.
8/13/2019 Hotuba Ya Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Mhe Joseph S. Warioba, Ripoti ya Tume kwa Rais Kikwet
6/23
6
Hii ni mara ya kwanza kwa nchi yetu kuwashirikisha kwa ukamilifu
wananchi katika kutunga katiba ya nchi yao. Nia ya mchakato huu ni
kupata katiba inayokubalika na wananchi. Ili katiba ikubalike na wananchi
ni jambo la msingi maoni yao yapewe uzito unaostahili. Nayasema haya
kwa sababu tangu Rasimu ya kwanza itolewe maeneo yaliyopewa uzito
na wananchi hayakupewa uzito katika mijadala ya viongozi, wasomi na
vyombo vya habari.
Mheshimiwa Rais,
Utangulizi wa Katiba unaeleza kuwa Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania imetungwa na Wananchi wa Tanzania. Utangulizi
unatoa taswira na picha halisi ya Jamhuri ya Muungano na watu wake,
historia yao, matarajio yao, misingi ya taifa na masuala muhimu ambayo
Wananchi wanataka kuyaendeleza katika jamii, kizazi hadi kizazi.
Sura ya Kwanza inaelekeza kuendelea kuwepo kwa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania. Yapo pia masharti kuhusu alama za Taifa na
sikukuu za Taifa na Rasimu inatambua Lugha ya Kiswahili kuwa Lugha ya
Taifa. Imeainisha pia tunu za Taifa ambazo ni Uhuru, Haki, Udugu,
Amani, Usawa, Umoja na Mshikamano. Tunu za Taifa ndiyo msingi wa
maadili na taratibu mbalimbali za kimaisha za jamii mbali mbaliambazo
hurithishwa kizazi hadi kizazi.
8/13/2019 Hotuba Ya Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Mhe Joseph S. Warioba, Ripoti ya Tume kwa Rais Kikwet
7/23
7
Mheshimiwa Rais,
Dira ya Taifa ni eneo ambalo wananchi walilitolea maoni kwa wingi
na kwa uzito. Sura ya Pili ya rasimu kuhusu malengo muhimu, misingi ya
mwelekeo wa shughuli za Serikali na sera za kitaifa imejumuisha maoni
mengi ya wananchi. Wakulima, wafugaji, wavuvi na makundi mengine
wanataka kuwe na dira ya Taifa ambayo ndiyo itakuwa mwongozo mkuu
utakaofuatwa na kuzingatiwa na uongozi, hasa Serikali na vyama vya
siasa katika kutekeleza shughuli za kisiasa, kiuchumi, kijamii, kiutamaduni
na kimazingira.
Sura ya Tatu imependekeza masharti kuhusu Maadili na Miiko ya
Uongozi na Utumishi wa Umma. Uongozi ni dhamana, na kiongozi wa
Umma anatakiwa kutekeleza wajibu wake kwa kuheshimu Wananchi,
kukuza hadhi ya Taifa na kukuza imani na heshima ya Utumishi wa Umma
kwa Wananchi. Rasimu imeorodhesha miiko ya uongozi ikiwa ni pamoja
na kupiga marufuku kiongozi wa Umma kutumia wadhifa, nafasi ya
madaraka au cheo chake kwa manufaa yake binafsi, familia yake, ndugu,
jamaa, marafiki au mtu yeyote aliye na uhusiano naye wa karibu.
Mheshimiwa Rais,
Sura ya Nne, inahusu Haki za Binadamu, Wajibu wa Raia na
Mamlaka za Nchi. Wananchi wametoa maoni mengi kuhusu haki za
8/13/2019 Hotuba Ya Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Mhe Joseph S. Warioba, Ripoti ya Tume kwa Rais Kikwet
8/23
8
binadamu na hasa katika suala la utekelezaji na usimamizi wa haki hizo.
Kutokana na maoni ya Wananchi, Rasimu imeboresha haki za binadamu
zilizomo katika Katiba ya sasa na kuongeza haki mpya za mtu binafsi na
haki za makundi mbalimbali kama vile watoto, wanawake, wazee, vijana,
makundi madogo katika jamii, watu wenye ulemavu, wafanyakazi, waajiri
na haki ya kutafuta, kutoa na kusambaza habari. Aidha, Rasimu
imeainisha wajibu wa raia ikiwa ni pamoja na kulinda na kutetea Katiba
na Sheria za Nchi; kulipa kodi, kuheshimu haki, uhuru na maslahi ya watu
wengine na kulinda na kutunza mazingira.
Sura ya Tano inahusu Uraia wa Jamhuri ya Muungano. Uraia ni
mmoja, nao ni wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Rasimu ya Katiba
inapendekeza kutambuliwa kwa uraia wa kuzaliwa na kujiandikisha
ambao ni wa nchi moja. Aidha, Rasimu inapendekeza kuwapa hadhi
maalum watu wenye asili au nasaba ya Tanzania ambao wameacha kuwa
raia wa Tanzania kwa kuchukua uraia wa nchi nyingine.
Mheshimiwa Rais,
Kuhusu Serikali ya Jamhuri ya Muungano, Rasimu ya Katiba
imefafanua kwa kina na ufasaha juu ya Rais wa Jamhuri ya Muungano
ambaye ni alama na taswira ya nchi na Watu wake. Yeye peke yake
ndiye mwenye hadhi na heshima ya Mkuu wa Nchi, Amiri Jeshi Mkuu na
8/13/2019 Hotuba Ya Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Mhe Joseph S. Warioba, Ripoti ya Tume kwa Rais Kikwet
9/23
9
Kiongozi wa Serikali. Kwa kuzingatia maoni ya Wananchi, madaraka ya
Rais na hasa yale ya uteuzi yamepunguzwa kwa kuweka vyombo vya
kupendekeza majina ya Watu wa kuteuliwa na kwa baadhi ya vyeo
kuhitaji kuthibitishwa na Bunge.
Mheshimiwa Rais,
Wananchi wametaka Katiba itambue mamlaka na madaraka yao
juu ya wawakilishi wao katika Bunge, na kama ilivyokuwa katika Rasimu
ya Awali, inapendekezwa Wabunge wasiwe Mawaziri, kuwe na ukomo wa
uwakilishi katika Bunge na wapiga kura wawe na madaraka ya
kumwajibisha Mbunge hata kabla ya kumalizika kwa muhula wake na
Spika na Naibu Spika wasitokane na Wabunge au kiongozi wa juu wa
chama cha siasa.
Kuhusu Mahakama ya Jamhuri ya Muungano, Sura ya Kumi imebaki
na mapendekezo ya awali ya kuanzishwa kwa Mahakama ya Juu
(Supreme Court) na kuendelea kuwepo kwa Mahakama ya Rufani. Aidha,
inapendekezwa, kama ilivyo katika Katiba ya sasa, Mahakama Kuu ya
Tanzania Bara (Tanganyika) na Mahakama Kuu ya Zanzibar, ziendelee
kuwa na mamlaka sawa ya kusikiliza katika ngazi ya awali, mashauri ya
madai na jinai yanayohusu sheria za Serikali ya Jamhuri ya Muungano
katika maeneo yao ya utawala (concurrent jurisdiction).
8/13/2019 Hotuba Ya Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Mhe Joseph S. Warioba, Ripoti ya Tume kwa Rais Kikwet
10/23
10
Mheshimiwa Rais,
Tume kwa kuzingatia maoni ya Wananchi, tofauti na ilivyokuwa
katika Rasimu ya Awali, sasa inapendekeza Msajili wa Vyama vya Siasa
iwe ni taasisi inayojitegemea na siyo kuwa Sehemu ya Tume Huru ya
Uchaguzi.
Kuhusu ulinzi na usalama, Sura ya Kumi na Tano inatamka kuwa
jukumu la ulinzi na usalama wa Jamhuri ya Muungano ni la kila raia.
Kwa kuzingatia maoni ya Wananchi waliyoyatoa katika Mabaraza ya
Katiba, Rasimu sasa inapendekeza kuwepo kwa Jeshi la Polisi moja na
Idara ya Usalama wa Taifa moja katika Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania.
Mheshimiwa Rais,
Mabadiliko makubwa ya Katiba lazima yaendane na masharti
yatokanayo na Masharti ya Mpito ambayo nayo ni sehemu ya Katiba.
Masharti haya yanaweka utaratibu, mfumo wa kikatiba na kisheria kuhusu
masuala ya kiutawala, uongozi wa nchi, sheria za nchi, nafasi za
madaraka na namna mambo yote hayo yatakaavyokuwa na kuendeshwa.
Sura ya Kumi na Saba inapendekeza Muda wa Mpito wa Miaka
Minne, kuanzia tarehe ya kuanza kutumika kwa Katiba Mpya hadi tarehe
31 Desemba, 2018. Katika kipindi hicho, sheria zilizopo hivi sasa
8/13/2019 Hotuba Ya Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Mhe Joseph S. Warioba, Ripoti ya Tume kwa Rais Kikwet
11/23
11
zitaendelea kutumika hadi zitakapobadilishwa. Sheria zinazotumika
Tanzania Bara zitakuwa za Tanganyika na sheria zinzotumika Tanzania
Bara na Zanzibar zitakuwa Sheria za Jamhuri ya Muungano. Yapo pia
mapendekezo kuhusu masuala ya kufanyiwa kazi katika Muda wa Mpito.
Mambo haya ni pamoja na:-
(i) Kutungwa kwa Katiba ya Tanganyika;(ii) Kurekebisha Katiba ya Zanzibar ya Mwaka 1984 ili kuwiana
na masharti ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ya mwaka 2014;
(iii) Mgawanyo wa rasilimali baina ya Serikali ya Jamhuri yaMuungano na Serikali za Nchi washirika;
(iv) Kuundwa kwa Tume na Taasisi za Kikatiba zilizoainishwakwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya
Mwaka 2014 na kwa kuzingatia masharti ya Katiba hiyo;
(v) Kufanya maandalizi na kuendesha Uchaguzi Mkuu waMwaka 2015 kwa kuzingatia masharti ya Katiba ya Jamhuri
ya Muungano ya Mwaka 2014; na
(vi) Kufanya maandalizi ya mambo yote muhimu kwa ajili yautekelezaji bora wa masharti ya kikatiba yaliyomo kwenye
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka
2014.
8/13/2019 Hotuba Ya Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Mhe Joseph S. Warioba, Ripoti ya Tume kwa Rais Kikwet
12/23
12
Mheshimiwa Rais,
Moja ya mambo ambayo yamejadiliwa sana na kwa hisia kali tangu
Rasimu ya awali ilipotolewa na Tume ni Muungano wa Tanzania. Jambo
kubwa limekuwa juu ya muundo wa Muungano. Wakati Tume inazindua
Rasimu ya Awali tulisema hatukupendekeza kuendelea kuwa na muundo
wa Serikali mbili kwa sababu mbalimbali. Tulisema kuwa kuendelea kwa
Serikali mbili kulihitaji ukarabati mkubwa ambao tulifikiri hautawezekana.
Mabaraza ya Katiba yalitoa maoni mengi ambayo yaliilazimu Tume
kufanya tena uchambuzi wa kina. Kama ilivyokuwa katika Rasimu ya
Awali, suala la muundo wa Muungano ndilo lililochukuwa muda mwingi
wa Tume. Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ilielekeza kwamba Tume
itaongozwa na misingi mikuu ya kitaifa na maadili ya jamii ya kuhifadhi na
kudumisha mambo kadhaa. Moja ya mambo hayo ilikuwa ni kuwepo kwa
Jamhuri ya Muungano. Hivyo, Tume ilianza kazi kwa madhumuni ya
kupata maoni ya kuboresha Muungano. Wananchi wengi walitoa maoni
kuhusu Muungano, lakini wengi wao walijikita kwenye Muundo wake.
Kwa Tanzania Bara, wananchi zaidi ya 39,000 walitoa maoni kuhusu
Muungano na kati ya hao, karibu 27,000 walizungumzia muundo. Kwa
Zanzibar, wananchi karibu wote waliotoa maoni walijikita kwenye suala la
Muungano. Kati ya wananchi karibu 38,000 waliotoa maoni Wananchi
19,000 walitoa maoni kuhusu muundo wa Muungano.
8/13/2019 Hotuba Ya Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Mhe Joseph S. Warioba, Ripoti ya Tume kwa Rais Kikwet
13/23
13
Mchanganuo wa takwimu hizi unaonyesha kuwa kwa upande wa
Tanzania Bara, 13% walipendelea Serikali moja, 24% walipendekeza
Serikali mbili na 61% walipendekeza Serikali tatu. Kwa upande wa
Zanzibar, 34% walipendekeza Serikali mbili na 60% walipendekeza
Muungano wa Mkataba, na 0.1% (watu 25) walipendekeza Serikali moja.
Aidha, taasisi nyingi kama vile vyama vya siasa, asasi za kiraia na jumuia
za kidini zilipendekeza muundo wa Serikali tatu. Baadhi ya taasisi za
kiserikali, ama moja kwa moja au kwa tafsiri ya mapendekezo yao, pia
zilipendekeza Serikali tatu. Kwa mfano, Baraza la Wawakilishi Zanzibar
lilipendekeza kuwepo kwa mamlaka huru ya Zanzibar, mamlaka huru ya
Tanganyika na mamlaka ya Muungano na iwekwe wazi maeneo, uwezo,
nguvu, utendaji na mipaka ya kila mamlaka. Ofisi ya Waziri Mkuu
imependekeza mfumo wa serikali tatu ili kuondoa kero za muungano.
Aidha, Mamlaka ya Mapato Tanzania imependekeza kuwepo kwa Serikali
tatu ili kutoa majibu ya kero zilizopo na kuleta utulivu zaidi ilimradi
upangiliwe vizuri.
Mheshimiwa Rais;
Baada ya kuona takwimu hizi na kuchanganua sababu zilizotolewa
na makundi mbali mbali, Tume iliamua kufanya utafiti kuhusu muundo wa
Muungano. Suala hili lilijitokeza kwa nguvu na hisia kali mara ya kwanza
mwaka 1984 katika kipindi kilichoitwa kuchafuka kwa hali ya hewa
8/13/2019 Hotuba Ya Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Mhe Joseph S. Warioba, Ripoti ya Tume kwa Rais Kikwet
14/23
14
kisiasa Zanzibar. Mwaka 1991 Tume ya Nyalali ilipendekeza Muundo wa
Serikali tatu. Miaka miwili baadaye, yaani Mwaka 1993, kikundi cha
Wabunge wa Tanzania Bara katika Bunge la Muungano, G55,
kilipendekeza kuwa na muundo wa Serikali tatu na Bunge likaridhia.
Mwaka 1999 Kamati ya Kisanga ilipendekeza muundo wa Serikali tatu.
Tume pia imepitia taarifa ya Kamati nyingi zilizoundwa na Serikali ya
Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kama vile,
Kamati ya Amina Salum Ali na Kamati ya Shelukindo ya mwaka 1994.
Sababu zilizotolewa katika matukio hayo ya mwanzo kwa kiwango
kikubwa, zinafanana na zile ambazo zimetolewa kipindi hiki. Kila upande
wa Muungano una malalamiko mengi kuhusu muundo wa Muungano.
Katika Taarifa ya Tume tunayokukabidhi leo, tumeorodhesha malalamiko
kumi kwa upande wa Zanzibar na malalamiko manane kwa upande wa
Tanzania Bara. Kwa upande wa Zanzibar malalamiko matatu makubwa
ni;
(i) Serikali ya Tanganyika imevaa koti la Serikali ya Muunganoambalo linaisaidia Tanganyika zaidi kuliko Zanzibar. Koti hilo
limeifanya Tanganyika kuwa ndiyo Tanzania;
(ii) Mambo ya Muungano yamekuwa yakiongezeka na hivyokuathiri madaraka ya Zanzibar (autonomy) na kufifisha hadhi
ya Zanzibar (identity) na Zanzibar inaendelea kumezwa; na
8/13/2019 Hotuba Ya Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Mhe Joseph S. Warioba, Ripoti ya Tume kwa Rais Kikwet
15/23
15
(iii) Kumwondoa Rais wa Zanzibar kuwa Makamu wa Rais waJamhuri ya Muungano.
Kwa upande wa Tanzania Bara, malalamiko makubwa ni;
(i) Zanzibar imekuwa nchi huru, ina bendera yake, ina wimbowake wa Taifa ina Serikali yake na imebadili Katiba yake ili
ijitambue kama nchi, wakati Tanzania Bara imepoteza
utambulisho wake. Katiba ya Jamhuri inasema Tanzania ni
nchi moja lakini Katiba ya Zanzibar inasema ni nchi mbili;
(ii) Zanzibar imebadili Katiba yake na kuchukua madaraka yaJamhuri ya Muungano, kama vile kuelekeza sheria za
Muungano zilizopitishwa na Bunge la Muungano zipelekwe
kwenye Baraza la Wawakilishi. Maana yake ni kuwa Katiba ya
Zanzibar sasa ipo juu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano; na
(iii) Wananchi wa Tanzania Bara kutokuwa na haki ya kumilikiardhi Zanzibar wakati wenzao wa Zanzibar wana haki hiyo
Tanzania Bara.
Mheshimiwa Rais;
Katika kuchambua malalamiko ya Zanzibar kwamba Tanganyika
imevaa koti la Muungano, Tume imebaini kwamba muundo wa Muungano
wa Serikali mbili umeifanya Serikali ya Muungano kwa kiwango kikubwa
8/13/2019 Hotuba Ya Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Mhe Joseph S. Warioba, Ripoti ya Tume kwa Rais Kikwet
16/23
16
kushughulikia zaidi mambo ya Tanzania Bara, hasa mambo ya
maendeleo. Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka
1977, Serikali ya Muungano ina mamlaka ya kusimamia mambo ya
muungano na mambo yasiyo ya muungano kwa upande wa Tanzania
Bara. Kwa msingi huo, Serikali ya Muungano inashughulikia sana mambo
ya kilimo, elimu, afya, maji, nishati na madini, ujenzi, uchukuzi, maliasili
na utalii na mengine ya Tanzania Bara ambayo siyo mambo ya
Muungano. Wakati wa kikao cha Bajeti Bunge la Muungano hutenga siku
mbili au tatu za majadiliano kwa Wizara zinazosimamia mambo haya
yasiyo ya Muungano ya Tanzania Bara wakati mambo ya Muungano kama
vile ulinzi, mambo ya nje na mambo ya ndani hutengewa siku moja au
nusu siku. Maswali ya Wabunge kuhusu mambo ya maendeleo pia
yanahusu Tanzania Bara na ziara za Wabunge kukagua miradi ya
maendeleo zinahusu Tanzania Bara katika mambo yasiyo ya Muungano.
Mambo haya Bungeni yanasimamiwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya
Muungano ambaye, kihalisia hana mamlaka wala madaraka yoyote
kuhusu Zanzibar.
Aidha, muundo huu wa muungano pia umesababisha kuwepo kwa
wizara au taasisi zenye sura au zinazotekeleza mambo ya muungano
pekee; mambo ya Tanzania Bara na mambo mchanganyiko; kwa maana
ya mambo ya muungano na mambo yasiyo ya muungano, hali ambayo
8/13/2019 Hotuba Ya Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Mhe Joseph S. Warioba, Ripoti ya Tume kwa Rais Kikwet
17/23
17
inapekea ugumu wa kutofautisha gharama za muungano na zisizo za
muungano katika wizara au taasisi hizo. Kundi la pili na la tatu ndio
imekuwa chanzo cha kero za muungano.
Hakuna njia ya kubadili hali hii kwa sababu Serikali ya Muungano
haina mamlaka ya kutoshajuu ya mambo ya maendeleo kwa upande wa
Zanzibar. Mawaziri wengi na Serikali kwa ujumla inalazimika kupanga
maendeleo na kutafuta rasilimali kwa ajili ya Tanzania Bara zaidi kuliko
kwa Zanzibar. Zanzibar hufanya mipango yake ya maendeleo. Lakini, ili
kupata rasilimali kama mikopo na misaada ni lazima ipitie Serikali ya
Muungano, jambo ambalo utekelezaji wake umesababisha matatizo
mengi. Utatuzi wa matatizo hayo umekuwa mgumu, umechukua muda
mrefu au umeshindikana. Njia pekee ambayo ingefanya maendeleo ya
Zanzibar yapewe uzito sawa na mambo ya Tanzania Bara ni kuyaweka
mambo hayo chini ya Serikali ya Muungano, yaani kuwa na Serikali moja.
Hata hivyo, hilo likifanyika kuna hofu ya Zanzibar kumezwa.
Mheshimiwa Rais;
Tume imefanya uchambuzi wa ndani kuhusu malalamiko ya
Zanzibar kwamba kuongezeka kwa Mambo ya Muungano kumeathiri
madaraka ya Zanzibar (autonomy). Tangu mwanzo wa Muungano,
ilikubalika kwamba Zanzibar ibaki na hadhi yake na iwe na madaraka
8/13/2019 Hotuba Ya Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Mhe Joseph S. Warioba, Ripoti ya Tume kwa Rais Kikwet
18/23
18
kuhusu Mambo yasiyo ya Muungano. Tume ilifanya uchambuzi wa Mambo
ya Muungano ili kubaini kama yanaingilia hadhi na uhuru wa Zanzibar.
Kati ya Mambo 22 ya Muungano, Tume imebaini kuwa siyo mambo yote
yanatekelezwa kikamilifu kimuungano. Mambo mengi yamebadilishwa bila
ya kubadili katiba, ama kwa makubaliano kati ya pande zote mbili za
Muungano au kwa hatua zilizochukuliwa na upande mmoja. Mambo hayo
ni pamoja na kodi, bandari, leseni za viwanda, usafiri na usafirishaji wa
anga, utafiti, posta na simu, uraia, takwimu, mafuta na gesi na
Mahakama ya Rufani.
Kwa hali halisi ilionekana hakuna uwezekano kuyarudisha kwenye
orodha ya muungano mambo ambayo yameondolewa kiutekelezaji.
Kwa kipindi cha miaka ishirini iliyopita, Kamati nyingi zimeundwa na
kutoa mapendekezo ya kuondoa mambo mengi zaidi kutoka kwenye
Orodha ya Mambo ya Muungano, ikiwa ni pamoja na elimu ya juu,
biashara ya nje, uhusiano wa kimataifa, mikopo, misaada ya nje na
mafuta na gesi. Wakati Tume inakusanya maoni, Wananchi wengi wa
Zanzibar kutoka makundi mawili makubwa, yaani wale waliotaka
Muungano wa Serikali Mbili na wale waliotaka Muungano wa mkataba,
wote walipendekeza mambo hayo yaondolewe kwenye Orodha ya Mambo
ya Muungano.
8/13/2019 Hotuba Ya Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Mhe Joseph S. Warioba, Ripoti ya Tume kwa Rais Kikwet
19/23
19
Kwa tathmini ya Tume baadhi ya mambo haya hakuna budi
yaondolewe kutoka orodha ya muungano la sivyo kero za muungano
zitaendelea. Kwa mfano suala la uhusiano wa kimataifa likiendelea kuwa
ni jambo la muungano Zanzibar haitaweza kujiunga na mashirika kama
OIC na FIFA. Kwa msingi huo, Tume imependekeza kuliondoa suala la
uhusiano wa kimataifa katika mambo ya muungano na kubakisha suala la
mambo ya nje.
Eneo jingine ni mgongano kati ya Katiba ya Muungano, na Katiba ya
Zanzibar. Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 imeweka masharti kwamba
sheria zinazotungwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano hazitatumika
Zanzibar hadi zipelekwe kwenye Baraza la Wawakilishi. Aidha, kodi
itakayoamuliwa na Bunge kutozwa na Serikali ya Muungano lazima ipate
ridhaa ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar.
Mambo haya yameleta mgongano wa Katiba. Juhudi zilizofanywa
na pande zote mbili hazikufanikiwa kuondoa mgongano huo. Zaidi ya
hapo, mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar yaliyofanywa mwaka 2010
yametamka wazi kwamba Zanzibar ni nchi kati ya nchi mbili za Muungano
wakati Katiba ya Jamhuri inaelekeza kwamba Tanzania ni Nchi moja.
Mabadiliko katika Katiba ya Zanzibar pia yamehamisha baadhi ya
madaraka ya Serikali ya Muungano kwenda Zanzibar.
8/13/2019 Hotuba Ya Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Mhe Joseph S. Warioba, Ripoti ya Tume kwa Rais Kikwet
20/23
20
Wakati wa kukusanya maoni ya wananchi, Tume ilibaini kwamba
haitakuwa rahisi kubadili Katiba ya Zanzibar kuifanya Zanzibar kuonekana
kuwa sehemu ya Jamhuri ya Muungano badala ya kuwa sura ya nchi
kamili. Mabadiliko ya aina hiyo yatahitaji kura ya maoni kama Katiba ya
Zanzibar inavyoelekeza. Kwa tathmini ya Tume, baada ya kuwasikiliza
wananchi wa Zanzibar, ni dhahiri kwamba pendekezo la kuifanya Zanzibar
isionekane kama nchi halitakubalika kwenye kura ya maoni.
Kwa kifupi tathimini yetu ni kwamba ukarabati mkubwa unahitajika
ili kuendelea na muundo wa Serikali mbili. Maeneo mawili makubwa
yanahitaji mabadiliko. Jambo la kwanza ni kuwa na mambo ya kutosha
kwenye orodha ya muungano, ikiwa ni pamoja na mambo ya maendeleo
na kiuchumi. Jambo hilo likifanyika, litazidisha malalamiko kwa upande
wa Zanzibar kuwa hadhi na madaraka yake yanazidi kupotea. Aidha,
Mambo ya muungano yakipunguzwa sana Serikali ya Muungano itakuwa
inashughulika zaidi na zaidi na mambo ya Tanganyika; na Zanzibar itaona
Tanganyika ndiyo muungano. Lakini kwaupande mwingine, Tanganyika
nayo itaona si haki nayo isiwe na uhuru wa kuendesha mambo yake kama
ilivyo kwa Zanzibar.
Jambo la pili ni kuondoa mgongano na mgogoro wa Katiba. Hiyo
maana yake ni Zanzibar kubadili Katiba yake ili Zanzibar na Tanganyika
ziwe ni sehemu za nchi moja badala ya kuwa nchi kamili. Kama Zanzibar
8/13/2019 Hotuba Ya Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Mhe Joseph S. Warioba, Ripoti ya Tume kwa Rais Kikwet
21/23
8/13/2019 Hotuba Ya Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Mhe Joseph S. Warioba, Ripoti ya Tume kwa Rais Kikwet
22/23
22
Pili ni Serikali ya Muungano kuwa na uhakika wa mapato kwa ajili ya
kulipia gharama za Muungano. Tume imependekeza ushuru wa bidhaa
uwe ni kodi ya Muungano. Kodi hii itakidhi sehemu kubwa ya matumizi
ya Muungano na sehemu itakayobaki itapatikana kutokana na mapato
yasiyo ya kodi yanayotokana na mambo ya muungano, michango ya Nchi
Washirika na mikopo. Tatu ni kuundwa kwa Tume ya Uhusiano na
Uratibu wa Serikali chini ya Uenyekiti wa Makamu wa Rais wa Muungano
na itajumuisha viongozi wakuu wa nchi washirika. Majukumu ya Tume
hiyo ni kusimamia mashauriano na mashirikiano kati ya Serikali ya
Muungano na Serikali za nchi washirika ili kuhakikisha sera zinawiana na
pia kusimamia na kuimarisha masuala yenye maslahi kwa taifa na pia
kutatua migogoro.
Mheshimiwa Rais;
Kazi hii haikuwa rahisi hata kidogo. Sisi wajumbe kila mmoja
tulikuwa tumetoka kwenye makundi tofauti tofauti. Kila mmoja wetu
alikuwa na imani yake, maono yake, itikadi yake, msimamo wake na
kadhalika. Lakini tulikubaliana mapema kabisa kwamba wajibu wetu ni
kwa taifa. Kwa hivyo, tuliacha imani na misimamo yetu binafsi na
kuamua kuwasikiliza wananchi kwa makini sana. Majadiliano yetu
yalilenga kupata mwafaka wa kitaifa. Matokeo yake ni maamuzi ya
maridhiano.
8/13/2019 Hotuba Ya Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Mhe Joseph S. Warioba, Ripoti ya Tume kwa Rais Kikwet
23/23
23
Baadhi ya mapendekezo yetu kwa hakika yatapokelewa kwa
hamasa kubwa. Lakini la muhimu ni kupata mwafaka wa kitaifa badala
ya kufikia uamuzi kwa kujipima katika makundi.
Baada ya kusema hayo machache lakini kwa maneno mengi, kwa
heshima kubwa, naomba sasa kwa niaba ya Tume, kama sheria
inavyoelekeza, nikukabidhi wewe Mheshimiwa Rais na Mheshimiwa Rais
wa Zanzibar, Ripoti ya Tume pamoja na Viambatanisho vyake Saba,
ikiwemo Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.