1
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
UFAFANUZI WA HOJA ZA WAHESHIMIWA WABUNGE
WAKICHANGIA HOTUBA YA WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO,
MHE. DKT. PHILIP I. MPANGO (MB), AKIWASILISHA BUNGENI
MAPENDEKEZO YA MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA
KWA MWAKA 2017/18 NA MWONGOZO WA KUANDAA
MPANGO NA BAJETI YA SERIKALI KWA
MWAKA 2017/18
DODOMA NOVEMBA, 2016
1
A. UTANGULIZI
1. Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua fursa hii kukushukuru
wewe binafsi, Naibu Spika na Wenyeviti wa Bunge kwa kuendesha
majadiliano kwa ufanisi kuhusu Mapendekezo ya Mpango wa
Maendeleo wa Taifa na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti kwa
Mwaka 2017/18.
2. Mheshimiwa Spika, napenda kutambua mchango mzuri
uliotolewa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, chini ya
Mwenyekiti wake Mhe. Hawa Abdulrahman Ghasia, Mbunge wa
Mtwara Vijijini na Makamu Mwenyekiti, Mhe. Josephat Sinkamba
Kandege, Mbunge wa Kalambo. Ninatambua pia mchango wa waziri
kivuli na msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu
wizara ya Fedha na Mipango, Mhe. Halima James Mdee, Mbunge wa
Kawe. Aidha, ninawashukuru kwa dhati Waheshimiwa Wabunge wote
waliochangia mjadala huu kwa kuzungumza (45) na kwa maandishi
(30).
3. Mheshimiwa Spika, kwa ujumla mjadala ulikuwa mzuri, baadhi
ya maoni yakitolewa kwa hisia kali. Mimi naamini kwamba kwa
kuzingatia umuhimu wa uchumi katika nchi ni jambo jema
tukachambua, tukabishana na hatimaye turidhiane juu ya
vipaumbele, mikakati na hatua stahiki za kukuz auchumi kwa namna
endelevu zitakazowezesha kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya
Maendeleo 2025.
4. Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia kuwa tumepokea michango
na hoja nyingi sana kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge, naomba
niahidi hapa kuwa nitawasilisha Bungeni taarifa ya maandishi
inayofafanua hoja zote zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge.
B. MAONI NA USHAURI ULIOSISITIZWA NA WAHESHIMIWA
WABUNGE WENGI
5. Mheshimiwa Spika, yapo maoni/ushauri mbalimbali uliotolewa
na Waheshimiwa Wabunge ambayo Serikali itazingatia katika
kuandaa Mpango wa Maendeleo na Bajeti kwa Mwaka 2017/18.
Ushauri huo ni:-
2
(i) Serikali ijielekeze kubuni vyanzo vingine vya mapato (Non-tax
revenue) vitakavyosaidia kugharamia Bajeti ya Serikali;
(ii) Serikali ipunguze kukopa zaidi kutoka vyanzo vya ndani;
(iii) Kukamilisha haraka zoezi la Sovereign Rating ili kuwezesha
kukopa kutoka vyanzo vya nje;
(iv) Ujenzi wa Reli ya Kati kutoka Dar – Tabora - Kigoma (km 1,251)
kwa Standard Gauge na matawi yake;
(v) TRA iandae mapema awamu ya pili ya ukusanyaji wa kodi ya
majengo katika halmashuri na miji midogo iliyosalia;
(vi) Kutenga fedha za kutosha za matumizi mengineyo (OC) kwa
mafungu husika ili kuweza kugharamia mpango wa Serikali
kuhamia Makao Makuu – Dodoma hususan kwa upande wa
malipo ya stahili za watumishi watakaohamishwa;
(vii) Kukamilisha mifumo ya ukusanyaji wa mapato ya Serikali kwa
njia za kielektroniki;
(viii) Kuhamasisha na kuongeza matumizi ya mashine za EFD na
wananchi kwa ujumla kudai risiti halali pale wanaponunua
bidhaa;
(ix) Kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato hususan bandari bubu
na biashara za magendo;
(x) Kuboresha mazingira ya kufanya biashara na uwekezaji ili
kuiwezesha sekta binafsi kutoa mchango unaostahili katika
kukuza uchumi wa nchi yetu;
(xi) Kuweka mkakati wa kujenga zahanati katika kila kijiji na kituo
cha afya kwa kila kata na kuimarisha upatikanaji wa madawa
na vifaa tiba,
(xii) Kukamilisha utaratibu wa matumizi ya shilingi milioni 50 kwa
kila kijiji/mtaa/shehia na kuongeza kiasi kinachotengwa;
(xiii) Kuendeleza maeneo ya viwanda vidogo, na EPZ/SEZ;
(xiv) Kutoa kipaumbele kwa miradi ya makaa ya mawe - Mchuchuma
na chuma Liganga;
(xv) Kuboresha elimu ya juu na kuongeza wigo wa utoaji wa mikopo
kwa wanafunzi; na
(xvi) Kuendelea kuboresha miundombinu ya barabara.
3
C. UFAFANUZI WA HOJA MBALIMBALI
Hoja Na. 1: Uchumi una hali mbaya (Umedorora) na kuna
manung’uniko mengi ya wananchi mtaani.
Hali ya Uchumi (Januari – Juni 2016)
Ukuaji wa Pato la Taifa: 6.7% (Jan-Jun 2016) Vs 5.8% (Jan-
Jun 2015).
Sekta zilizokua zaidi: uchukuzi, uhifadhi wa mizigo (17.4%),
uchimbaji wa madini na gesi (13.7%), mawasiliano (13.0%) na
sekta ya fedha & bima (13.0%).
mfumuko wa bei: 6.5% (Jan 2016), 5.5% (Jun 2016) na 4.5%
(Sept 2016).
Akiba ya fedha za kigeni: 4 months of imports cover (USD 4.1
bn) Sept 2016
Urari wa Biashara ya Nje: current account deficit USD 601.8
(Jan – Sept 2016) Vs USD 1,207.7 (Jan – Sept 2015)
Mwenendo wa sekta ya kibenki (Januari – Septemba 2016).
Sekta imeendelea kukua na ina mitaji na ukwasi wa kutosha.
a) Mitaji ikilinganishwa na mali iliyowekezwa (Total Capital to Total
Risk Weighted Assets and Off-balance Sheet Exposures) ni
19.08% Vs kiwango cha chini kinachotakiwa 12.0%.
b) Mali inayoweza kubadilishwa kuwa fedha taslimu ikilinganishwa
na kiwango cha amana zinazoweza kuhitajika katika muda mfupi
(liquid assets to demand liabilities) 34.18% Vs kiwango cha chini
kinachohitajika 20%.
But: mikopo chechefu imeongezeka (6.7% Sept 2015, 9.1% Sept 2016)
Mabenki yaliyopata Hasara Jul – Sept 2016: CRDB & TIB
Development Bank.
Sababu: mikopo chechefu (provision for loan losses);
Twiga Bancorp imewekwa chini ya uangalizi wa BOT;
4
NB: Crane Bank Ltd ya Uganda imewekwa chini ya usimamizi wa
Benki Kuu Oct 2016; Imperial Bank Kenya, Oct 2015
Benki nyingi incl. CRDB na TIB Devt, zimekuwa na mitaji na ukwasi
wa kutosha. Matarajio ni kuwa benki hizi zitafanya vizuri katika
kipindi kilchobaki cha 2016/17.
Kwa mwaka ulioshia Sept 2016 Sekta ya Kibenki kwa ujumla
ilipata faida: pato kwa rasilimali (Return on Assets) 2.53%; pato kwa
mtaji (Return on Equity) 12.05%. Mtaji na kiwango cha mali inayoweza
kubadilishwa kuwa fedha taslimu Vs amana zinazoweza kuhitajika
katika muda mfupi (liquid assets to demand liabilities) viliendelea
kuwa juu ya viwango vinavyotakiwa.
Riba za mikpo zimepungua: 16.18% Sept 2015 – 15.83% Sept
2016
Riba za amana zilibakia wastani wa 9.0%;
Tofauti kati ya riba za mikopo na amana za mwaka mmoja ilipungua
1.77% pts (Sept 2016) kutoka 3.32 % pts (Sept 2015);
Mwenendo huu umeimarisha mazingira ya kufanya biashara na
ushindani.
Viwango vya Ubadilishaji fedha
Hatua za kuimarisha thamani ya Shilingi:
(i) kuongeza mauzo ya bidhaa nje;
(ii) kuimarisha uzalishaji wa nishati; na
(iii) kupunguza matumizi ya fedha za kigeni yasiyo na tija.
Wastani wa Shs. 2,172.38: USD 1 (Jan 2016), Shs. 2,180.54 (Jul
2016); Shs. 2,188.1: USD 1 (Sept 2016)
5
MWENENDO WA BAJETI YA SERIKALI
Bajeti2016/17
29,539,603,197,085
Matumizi ya Kawaida 17,719,100,237,510
CFS 8,010,400,471,000
MDAs 2,470,708,175,510
RSs 37,786,227,000
LGAs 332,039,536,000
LGAs own source 266,165,828,000
PE 6,602,000,000,000
Matumizi ya Maendeleo 11,820,502,959,575
Local 8,702,697,468,575
MDAs 7,993,548,468,575
RSs 55,000,000,000
LGAs 254,900,000,000
LGAs own source 399,249,000,000
Foreign 3,117,805,491,000
MDAs 2,518,396,820,000
RSs 10,940,832,000
LGAs 588,467,839,000
FedhazilizotolewaRoboya
kwanza Asilimia
5,464,422,947,958 18%
4,549,103,630,355 26%
2,293,670,167,443 29%
367,680,092,860 15%
16,416,804,465 43%
103,755,507,898 31%
64,400,691,531 24%
1,703,180,366,157 26%
915,319,317,603 8%
869,344,044,756 10%
798,787,466,850 10%
2,500,000,000 5%
11,000,000,000 4%
57,056,577,906 14%
45,975,272,847 1%
33,265,592,750 1%
690,672,965 6%
45,284,599,882 8%
Ulipaji wa Madeni ya Ndani
6. Mheshmiwa Spika, Katika kipindi cha Julai hadi Oktoba 2016
Serikali imelipa madeni mbalimbali yaliyohakikiwa na Mkaguzi wa
Ndani Mkuu wa Serikali yenye jumla ya shilingi bilioni 187.521.
Madeni haya yanajumuisha madeni ya wakandarasi wa barabara,
maji, umeme pamoja na wazabuni mbalimbali. Aidha, madeni ya
watumishi wa umma yanaendelea kulipwa kupitia mafungu yao.
Ulipaji wa Deni la Nje
7. Mheshimiwa Spika, Katika kipindi kuanzia Novemba 2015 hadi
kufikia Oktoba, 2016 Serikali imetumia jumla ya shilingi bilioni
1,196.9 kwa ajili ya kulipia madeni ya nje. Kati ya kiasi hicho, malipo
ya mtaji ni shilingi bilioni 709.7 na malipo ya riba ni shilingi bilioni
487.2. Malipo ya deni la Taifa yamekuwa yakiongezeka mwaka hadi
mwaka kutokana na mikopo mipya, kumalizika kwa kipindi cha kabla
ya kuanza kulipa mtaji (Grace Period) kwa mikopo ya muda mrefu
pamoja na kushuka kwa thamani ya shilingi dhidi ya Dola ya
6
Kimarekani.
8. Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kulipa kwa wakati
mikopo yote ya nje inayoiva kwa mujibu wa mikataba. Kwa kuwa
kutofanya hivyo kutahatarisha mahusiano yaliyopo kati yetu na nchi
wahisani, taasisi za fedha za kimataifa na mabenki ya nje. Aidha, nchi
isipolipa kwa wakati inaweza kushitakiwa kwenye mahakama za
kimataifa na kuisababishia nchi hasara na kupelekea kutopata
mikopo tena kutoka nje. Kadhalika, kutokulipa kwa wakati
kutasababisha Serikali kulipa gharama za ziada (penalty) kulingana
na makubaliano na hivyo kuongeza mzigo kwa taifa.
9. Mheshmiwa Spika, Serikali imejiwekea mikakati mbalimbali ili
kuhakikisha kwamba Deni la Taifa linadhibitiwa na linaendelea kuwa
himilivu na linalipwa kwa wakati.
Ruzuku ya Pembejeo za Kilimo
10. Mheshmiwa Spika, Katika mwaka wa fedha 2016/17 jumla ya
shilingi bilioni 25.0 zimetengwa kwa ajili ya ununuzi wa pembejeo
ambapo hadi kufikia mwezi Oktoba 2016 jumla ya shilingi bilioni 10.0
zimetolewa.
Ununuzi wa Chakula cha Hifadhi ya Taifa
11. Mheshmiwa Spika, Katika mwaka wa fedha 2016/17 jumla ya
shilingi bilioni 15.0 zimetengwa kwa ajili ya ununuzi wa chakula cha
hifadhi ya Taifa ambapo hadi kufikia mwezi Oktoba 2016 jumla ya
shilingi bilioni 9.0 zimetolewa.
Utoaji wa Fedha za Mfuko wa Jimbo
12. Mheshmiwa Spika, Katika mwaka wa fedha 2016/17 Serikali
imetenga shilingi bilioni 10.4 kwa ajili ya Mfuko wa Kuchochea
Maendeleo Jimboni. Kati ya fedha hizo shilingi bilioni 9.0 ni kwa ajili
ya Tanzania Bara na shilingi bilioni 1.4 ni kwa Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar. Serikali inatarajia kutoa fedha hizo mwezi Novemba
2016.
13. Mheshmiwa Spika, katika nusu ya kwanza ya mwaka 2016,
kasi ya ukuaji wa Pato la Taifa imeongezeka na kufikia asilimia 6.7
ikilinganishwa na asilimia 5.8 kwa nusu ya kwanza ya mwaka 2015.
7
14. Mheshimiwa Spika, manung’uniko mtaani yapo na kwa kiasi
kikubwa yametokana na jitihada na hatua zilizochukuliwa na Serikali
kurudisha nchi kwenye utaratibu wa nidhamu ya kazi katika
Utumishi wa Umma, kurejesha nidhamu ya matumizi/kuondoa
matumizi ya Serikali yasiyo ya lazima, kupambana na wizi/ubadhirifu
wa fedha na mali za umma, kuhimiza ulipaji kodi na ukusanyaji wa
mapato yasiyo ya kodi n.k. Hata hivyo, Serikali inaamini kuwa hatua
hizi ni kwa maslahi mapana ya Taifa na maumivu ni ya kipindi cha
mpito cha kuweka mambo sawa/kurejesha mifumo kwenye utaratibu
unaokubalika na endelevu. “There is no game without pain”.
15. Mheshimiwa Spika, upo utaratibu wa Serikali, Taasisi binafsi
na Mashirika ya Kimataifa kufanya tathmini ya uchumi wa nchi na
kutoa maoni yao juu ya kile walichokiona. Shirika la Fedha la
Kiamtaifa – IMF ambalo lilikuwa hapa wiki moja iliyopita,
limekamilisha tathmini ya mwenendo wa uchumi wa nchi yetu
ambapo kiujumla wameridhika na hali ya uchumi wa Tanzania.
Hoja Na. 2: Misingi ya Mpango (premises) iliyowekwa inatujengea
kushindwa.
16. Mheshimiwa Spika, neno ‘Misingi’ katika Mapendekezo ya
Mpango lililenga kumaanisha “assumptions”. Hakika Serikali inajua
kwamba hali halisi ya mazingia wezeshi kwa uwekezaji nchini na
nafasi ya Tanzania kama ilivyotathminiwa na Benki ya Dunia katika
Doing Business report. Serikali inajua utabiri wa hali ya hewa na
maoteo ya upungufu wa chakula n.k. We are not naïve. Assumptions
si lazima ziwe halisi bali ziliwekwa hapa kurahisisha uwekaji wa
malengo kwa mwaka 2017/18. Utaratibu huu ni wa kawaida kabisa
kwa wachumi. Mathalani tunapotaka kuchambua biashara baina ya
mataifa tunaweka assumption kwamba dunia ina nchi 2 tu zinafanya
biashara ili kurahisisha uchambuzi japo kila mtu anafahamu dunia
ina nchi nyingi zinafanya biashara baina yao.
Hoja na 3: Fedha kutopelekwa kwenye Halmashauri kwa wakati
17. Mheshmiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2016/17 Mamlaka
za Serikali za Mitaa ziliidhinishiwa bajeti ya shilingi bilioni 5,434.7.
Kati ya kiasi hicho shilingi bilioni 3,593.9 ni kwa ajili ya mishahara,
8
shilingi bilioni 598.2 ni kwa ajili ya matumizi mengineyo (OC)
ikijumuisha shilingi bilioni 266.2 za mapato yatokanayo na vyanzo vya
ndani vya Halmashauri na shilingi bilioni 332.0 ni ruzuku kutoka
Serikali Kuu. Aidha, shilingi bilioni 1,242.6 ni kwa ajili ya miradi ya
maendeleo ambapo shilingi bilioni 588.5 ni fedha za nje na shilingi
bilioni 654.1 ni fedha za ndani ikijumuisha shilingi bilioni 399.2
zinazotokana na mapato ya ndani ya Halmashauri na shilingi bilioni
254.9 ni ruzuku kutoka Serikali Kuu.
18. Mheshmiwa Spika, katika kipindi cha Julai hadi Oktoba 2016,
fedha zilizotolewa zinajumuisha mishahara shilingi bilioni 1,181.0
sawa na asilimia 33, matumizi mengineyo shilingi bilioni 192.8 sawa
na asilimia 32.2 na fedha za maendeleo shilingi bilioni 177.3 sawa na
asilimia 14.3. Aidha, mbali na fedha za ruzuku kutoka Serikali Kuu
na makusanyo ya ndani ya Halmashauri kiasi cha shilingi bilioni 271
zilitumika kutekeleza miradi ya maji vijijini (shilingi bilioni 51.1),
umeme vijijini (shilingi bilioni 132.4), Mfuko wa barabara (shilingi
bilioni 78.1) na utoaji wa pembejeo kwa wakulima (shilingi bilioni
10.0) katika Halmashauri mbalimbali nchini.
Hoja Na. 4: Mradi wa Mchuchuma na Liganga uko kwenye
Mpango wa maendeleo kila mwaka lakini utekelezaji wake
haujaanza
19. Mheshimiwa Spika, Sio kweli kuwa utekelezaji wa Mradi wa
Makaa ya Mawe, Mchuchuma na Chuma Liganga haujaanza.
Utekelezaji wa mradi huu utakaogharimu Dola za Marekani bilioni 3
umeanza na kufikia hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na:
Kukamilika kwa upembuzi yakinifu wa mradi ikiwa ni pamoja na
kutambua kiasi cha mashapo ya makaa ya mawe na chuma,
usanifu wa migodi na kiwanda cha chuma na kituo cha kuzalisha
umeme;
kupatikana kwa leseni za uchimbaji na matumizi ya madini,
leseni ya matumizi ya maji na leseni ya uzingativu wa mazingira;
Kukamilika pia kwa mkakati wa ushirikishi wa wananchi
wanaouzunguka mradi na njia ya kusafirishia umeme;
Kukamilika kwa ujenzi barabara kwa kiwango cha changarawe ili
kuruhusu usafirishaji wa mitambo kwenda kwenye eneo la mradi;
9
kuendelea na usanifu wa ujenzi wa reli ya liganga hadi Mtwara na
uwezekano wa kuiunganisha na reli ya TAZARA na kuendelea na
usanifu katika bandari ya Mtwara; na
kukamilika kwa tathmini ya fidia kwa wananchi watakaopisha
eneo la mradi imekamilika.
Hoja Na. 5: Utaratibu wa Taasisi za Umma kuweka fedha zao
katika Mabenki ya kibiashara urejeshwe ili kuwezesha mabenki
kukopesha fedha hizo kwa wafanyabishara na pia kuziwezesha
Taasisi hizo kunufaika na riba zitokanazo na amana.
20. Mheshimiwa Spika, uamuzi wa Serikali kuzitaka taasisi za
umma kufungua akaunti ya mapato Benki Kuu utaendelea kubaki
kama ulivyo. Utaratibu uliokuwa umejengeka ulizinufaisha benki
chache na haukuwa na maslahi mapana kwa Taifa. Benki hizo
zimekuwa zikipata faida kwa kutumia migongo ya maskini na hivyo
sasa basi! Benki zifanye kazi kwa kurejesha ushindani.
Mfano:
Taasisi moja ilikuwa na amana za muda maalum (fixed deposit) za
shilingi bilioni 440 ambazo ziliwekwa katika baadhi ya benki. Kiasi hiki
kilizaa faida ya shilingi bilioni 17 ambayo inamaanisha riba ya wastani
wa asilimia 4 kwa mwaka. Ijapokuwa ukweli ni kwamba, amana za
chini ya shilingi milioni 100 zinakuwa na riba ya kati ya asilimia 8 na
10 na kiasi cha amana kinapokuwa kikubwa zaidi riba inaongezeka
hadi kufikia asilimia 15. Kama riba ingekuwa asilimia 13, taasisi hiyo
ingepata faida ya bilioni 57.2 kabla ya kodi. Hivyo, kwa taasisi hiyo
moja tu, watanzania wamekuwa wakiibiwa shilingi bilioni 40 kila
mwaka.
Si hivyo tu, fedha hizo (bilioni 440) zilizokuwa katika benki za biashara
zilitumika kuikopesha Serikali kupitia hati fungani kwa riba ya asilimia
15, hivyo wananchi hulipa benki hizi riba ya hadi shilingi bilioni 66
kwa fedha ambazo ni za kwao wenyewe. Maana yake ni kuwa,
wananchi waliendelea kulipa riba kwa fedha zao wenyewe sawa na
hasara ya shilingi bilioni 106 kwa mwaka. Hatuwezi kuendelea na
utaratibu huu.
Benki na baadhi ya watanzania waliozoea kupiga dili sasa basi! Benki
ambazo zimekuwa zikipata faida kwa kutumia migongo ya maskini
10
sasa basi! Benki zifanye kazi kurejesha ushindani. Mheshimiwa Rais
alisema hadharani na ukweli utabaki hivyo, kwamba hizo fedha
hazitarudi.
Hoja Na. 6: Serikali ielekeze benki kushusha riba kutoka
asilimia 18 hdi 13 kwa wafanyabiashara wadogo na wakubwa
ili kuongeza mzunguko wa fedha katika uchumi. (Riba za
mikopo bado ziko juu, Serikali ielekeze benki kushusha riba
hizo)
21. Mheshimiwa Spika, Ni kweli riba za mikopo ni kubwa hasa zile
zinazotozwa na Taasisi ndogondogo za fedha (microfinance). Katika
Sekta ya Huduma Ndogo Ndogo za Fedha (Microfinance) kuna benki,
taasisi na asasi za fedha zilizo rasmi na zisizo rasmi ambazo zinatoa
huduma za kifedha kwa wateja wadogo wadogo. Pia kuna taasisi na
asasi za kifedha ambazo zinatoa huduma za mikopo kwa kutumia
mitaji binafsi bila kukusanya na kupokea amana za wateja.
22. Mheshimiwa Spika, Taasisi na asasi hizo zimeongezeka kwa
kiasi kikubwa na zimekuwa sehemu muhimu ya maendeleo ya
ujasiriamali na ukuaji wa uchumi wa wananchi na mikopo ya taasisi
hizo kwa kiasi kikubwa inategemewa na watanzania walio wengi.
23. Mheshimiwa Spika, Taasisi na asasi hizo zinapata leseni kutoka
katika mamlaka tofauti ikiwemo BRELA, Wizara ya Mambo ya Ndani
ya Nchi, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto, RITA, na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji.
Utaratibu huo umesababisha usimamizi na ufuatiliaji wa taasisi hizo
kuwa mgumu. Kutokana na hali hii zimejitokeza changamoto nyingi
na mapungufu kadhaa katika sekta ya “Microfinance”, ikiwa ni
pamoja na kutozwa riba kubwa na kuwa na mikataba yenye
mapungufu mengi. Hii inatokana na wakopeshaji kwenye sekta hii
kutokuwa na usimamizi imara na elimu ndogo ya maswala ya fedha
kwa wateja walio wengi (financial illiteracy).
24. Mheshimiwa Spika, Serikali inakiri kuwepo na malalamiko kwa
wananchi wengi nchini kuhusiana na uendeshaji wa biashara
inayofanywa na asasi hizo kama vile viwango vya juu vya riba na ada
pamoja na utaratibu mbaya wa ukusanyaji wa marejesho (loan
repayment). Hali hii inatokana na ukweli kwamba hakuna mamlaka
rasmi na halali ya kisheria yenye wajibu wa kutoa leseni, kuratibu,
11
kusimamia na kuhakikisha ulinzi wa wateja (consumer protection)
katika taasisi hizi za fedha.
25. Mheshimiwa Spika, Katika kutatua mapungufu na changamoto
hizi na kwa kuzingatia maendeleo yaliyojitokeza katika huduma za
fedha kwa wateja wadogo wadogo, Serikali imekamilisha na
kuidhinisha Sera ya Taifa ya ‘Microfinance’ na hatua za ukamilishaji
wa sheria ya Microfinance zinaendelea.
26. Mheshimiwa Spika, Sheria hiyo itaunda mfumo mahususi wa
kusimamia na kuratibu shughuli za taasisi na asasi za fedha zilizo na
zisizo rasmi ambazo zinatoa huduma za kifedha kwa wateja wadogo
wadogo ambazo haziko chini ya Sheria ya Mabenki na Taasisi za
Fedha ya mwaka 2006.
27. Mheshimiwa Spika, Kwa upande mwingine, benki na taasisi za
fedha zinazosimamiwa kisheria na Benki Kuu ya Tanzania,
zimeendelea kuwa na viwango bora vya riba katika kipindi cha mwaka
ulioishia mwezi Septemba 2016.
28. Mheshimiwa Spika, kuhusu kuweka riba elekezi, uzoefu wa
nchi nyingi unaonesha kwamba viwango vya riba huamuliwa na
nguvu ya soko. Ni dhamira ya Serikali kuona riba za benki
zinazotozwa katika mikopo zinapungu. Hivyo, Serikali itaendelea
kuweka mazingira mazuri yatakayosaidia kuleta ushindani
utakaopelekea viwango vya riba hizo kuwa nafuu zaidi. Aidha,
ikumbukwe kwamba kuna madhara ya kuweka viwango elekezi vya
riba ikiwa ni pamoja na uwezekano wa benki kupunguza mikopo kwa
sekta binafsi ikiwa kiwango hicho elekezi kitakuwa chini zaidi ya riba
ya dhamana na hati fungani za serikali; kuongezeka kwa mikopo
chechefu na kupungua kwa ushindani katika sekta ya benki na
ufanisi katika utekelezaji wa sera ya fedha.
Hoja Na. 7: TRA wanatumia vitisho, mabavu na mifumo
kandamizi katika kukusanya kodi
29. Mheshimiwa spika, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)
inaendelea na jitihada za kuhakikisha kila anayestahili kulipa kodi
analipa kodi stahiki na kwa wakati. TRA inatekeleza majukumu yake
12
kwa weledi na ufanisi kulingana na taratibu zilizoainishwa katika
sheria na kanuni za kodi.
30. Mheshimiwa spika, mlipakodi anakadiriwa kodi ya kulipa na
kupewa muda wa kuilipa kodi hiyo. Endapo kodi hiyo itakukuwa
haijalipwa katika muda ulioonyeshwa kwenye taarifa ya madai (Notice
of Assesment), TRA huchukua jukumu la kumkumbusha mhusika
(reminder notice) na kumtahadharisha hatua zitakazochukuliwa
endapo kodi hiyo itaendelea kutolipwa mpaka tarehe iliyooneshwa
kwenye reminder notice. Hatua zinazochukuliwa kwa mlipa kodi
aliyekaidi ni kama vile: kukamatwa mali zake na kuuzwa kwa njia ya
mnada; na kuiagiza benki ya mlipa kodi kuhamisha fedha kutoka
kwenye akaunti yake kwenda TRA ili kulipia deni hilo. Hatua hizi zipo
kwa mujibu wa sheria na si vitisho, mabavu wala mifumo kandamizi
kwa wafanyabiashara. Ni vizuri walipakodi wakazingatia sheria na
kulipa kodi kwa hiari ili kuepuka usumbufu.
Hoja Na. 8: Serikali inasema kuwa imeokoa shilingi bilioni 19
kwa kuondoa watumishi hewa kwenye mfumo wa maliopo.
Taarifa ya gharama za watumishi ya Benki Kuu ya Juni 2015
ilionyesha malipo ya mishahara yaliongezeka kutoka bilioni
456 hadi shilingi bilioni 534 Juni 2016 ambalo ni ongezeko la
bilioni 78. Ongezeko hili limetoka wapi wakati Serikali
imesimamisha ajira mpya na kuondoa watumishi hewa?
31. Mheshimiwa spika, Zoezi la kufuta watumishi hewa kufuatia
agizo la Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
lilianza Mwezi Machi, 2016. Hata hivyo, pamoja na kufutwa kwa
watumishi hewa malipo ya mishahara katika kipindi cha Juni 2015
hadi Juni 2016 yameongezeko kutokana na sababu mbalimbali
ikiwemo:
Nyongeza ya mishahara iliyoanza kutumika Julai, 2015 ambapo
jumla ya Shilingi bilioni 59 ziliongezeka kwa mwezi;
Watumishi 25,517 waliajiriwa katika kipindi hicho wenye
mshahara wa Shilingi bilioni 16.4 kwa mwezi;
Uwianishaji wa mishahara ya watumishi wa Vyuo Vikuu ambapo
jumla ya Shilingi bilioni 2.9 ziliongezeka;
Ongezeko la posho zinazoambatana na mishahara shilingi bilioni
6.1 kwa mwezi kwa vyombo vya ulinzi na usalama;
13
Upandishwaji vyeo kwa watumishi mbalimbali; na
Uwianishaji wa maeneo ya kimishahara ambapo kuanzia mwezi
Februari, 2016 mishahara ya shilingi bilioni 33 iliyokuwa
inalipwa kupitia kwenye kasma ya matumizi mengineyo ilianza
kulipwa kupitia kwenye kasma ya mishahara.
32. Mheshimiwa spika, Hivyo, endapo watumishi hewa
wasingeondolewa matumizi ya Serikali katika eneo la mishahara
yangekewa makubwa zaidi ya kiasi hicho kilicholipwa mwezi Juni,
2016.
Hoja Na. 9: Riba kubwa zinazotozwa na mabenki ni kandamizi
na zinaumiza wanyonge
33. Mheshimiwa spika, Katika mwaka ulioshia mwezi Septemba
2016, riba za mikopo za mabenki zimekuwa zikipungua wakati zile za
amana kuimarika kwa viwango tofauti. Riba za mikopo zilipungua
hadi kufikia wastani wa asilimia 15.83 mwezi Septemba 2016 kutoka
asilimia 16.18 mwezi Septemba 2015. Wakati huo huo, riba za amana
zilibakia katika kiwango cha wastani wa asilimia 9.0. Aidha, riba za
mikopo ya mwaka mmoja ilipungua kutoka wastani wa asilimia 14.27
hadi asilimia 13.23, wakati riba za amana za mwaka mmoja
ziliongezeka kutoka asilimia 10.95 hadi asilimia 11.46. Hali hii ilifanya
tofauti kati ya riba za mikopo na amana za mwaka mmoja ipungue
hadi kufikia wastani wa asilimia 1.77 mwezi Septemba 2016 kutoka
asilimia 3.32 mwezi Septemba 2015. Mwenendo huu wa viwango vya
riba unaonesha kuendelea kuimarika kwa mazingira ya kufanya
biashara na ushindani nchini hivyo kuvutia zaidi uwekezaji wa sekta
binafsi. Aidha, hii inaashiria kuimarika kwa ushindani wa Mabenki ili
kuvutia wateja.
14
MAJIBU YA HOJA ZA WAHESHIMIWA WABUNGE WAKATI WA KUJADILI MAPENDEKEZO YA MPANGO WA
MAENDELEO WA TAIFA KWA MWAKA 2017/18 NA MWONGOZO WA KUANDAA MPANGO NA BAJETI YA
SERIKALI KWA MWAKA 2017/18
NA. MTOA HOJA HOJA UFAFANUZI WA HOJA
KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI
1. TRA inavuka lengo
kutokana na kukusanya
maduhuli na
kuyahesabu kama
sehemu ya mapato ya
kodi.
Maelezo yaliyotolewa na Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
siyo sahihi.
Maelezo sahihi ni kuwa mapato ya kodi yanayokusanywa na
TRA hutolewa taarifa peke yake. Mapato yasiyo ya kodi
(maduhuli) kwa Mashirika ya Umma na Taasisi za Serikali
yanayokusanywa na Taasisi husika na kutolewa taarifa na
Msajili wa Hazina. Mapato yanayokusanywa na Wizara
hutolewa taarifa na Wizara husika.
WAHESHIMIWA WABUNGE
2. Mhe.
Josephat
Sinkamba
Kandege
Pamoja na lengo zuri la
kuongeza mapato ya
ndani ili ku kugharamia
sehemu kubwa ya bajeti,
Serikali ihakikishe kuwa
vyanzo vipya vya kodi
vinavyopendekezwa
Serikali inaendelea kutekeleza azma yake ya kupunguza
kodi zinazoleta kero kwa wananchi na kuharibu mpango
mkakati wa Serikali kuchochea ari ya ulipaji kodi kwa
hiari.
Aidha, Serikali imejikita katika kuimarisha mkakati wa
kuboresha usimamizi na utawala wa kodi ili
wafanyabiashara na wananchi waweze kulipa kodi
15
NA. MTOA HOJA HOJA UFAFANUZI WA HOJA
katika bajeti ya mwaka
wa Fedha 2017/18
havitakuwa kero kwa
wafanyabiashara na
wananchi wote kwa
ujumla.
zilizopo kwa hiari kwa maendeleo ya taifa lao.
3. Mhe. Ahmed
Ally Salum
Mabenki yanapata
hasara kutokana na
kupungua mzunguko wa
fedha. Serikali ichukue
hatua kwani endapo
mabenki yatafungwa
kutakuwa na athari
katika uchumi wa nchi
Katika kipindi cha Julai hadi Septemba 2016, baadhi ya
mabenki ya biashara yalipata faida ndogo na baadhi
zilipata hasara ikilinganishwa na kipindi kama hicho
mwaka uliotangulia. Hali hii imeathiri kasi ya utoaji
mikopo na hivyo kupunguza mzunguko wa fedha.
Miongoni mwa sababu zilizochangia hali hiyo ni pamoja
na Serikali kubaini watumishi hewa ambao miongoni
mwao walikopa kwenye mabenki na hivyo kusababisha
kuwepo kwa mikopo chechefu; serikali kuhamisha fedha
za mashirika ya umma kutoka katika mabenki ambazo
zilikuwa zinatumika kukopeshea; na hatua ya serikali ya
kubana matumizi yasiyo ya lazima kama vile kufanya
mikutano katika mahoteli. Aidha, fedha zilizotumika
kugaramia mikopo chechefu (provision for loan losses)
zilipelekea baadhi ya benki kupata hasara na nyingine
kupata faida kidogo.
Hata hivyo, hali hii ni ya mpito na Serikali inashauri
16
NA. MTOA HOJA HOJA UFAFANUZI WA HOJA
mabenki ya biashara kubuni mikakati ya kuongeza
amana zao ili kuongeza uwezo wa kukopesha. Aidha,
mabenki ya biashara yanatakiwa kuendelea kutumia
mfumo wa upashanaji taarifa za wakopaji (Credit
Reference System) ili kupunguza uwezekano wa
kuongezeka kwa mikopo chechefu.
17
HITIMISHO
34. Mheshimiwa Spika, napenda kuwashukuru Waheshimiwa
Wabunge wote waliochangia na kutupatia ushauri kuhusu
vipaumbele na mambo muhimu ya kuzingatia katika kazi inayofuata
ya kuandaa Mpango na Bajeti ya Mwaka 2017/18.
35. Mheshimiwa Spika, napenda niliahidi Bunge lako Tukufu
kwamba, Serikali itazingatia ushauri tuliopokea kwa kadri
inavyowezekana. Hakika haitawezekana kuzingatia kila kitu
kilichosemwa hapa. Baadhi yataendelea kuzingatiwa katika mipango
ya maendeleo itakayofuata. Ili Bunge lione wazi kwamba Serikali
inasikia na inathamini ushauri mzuri wa Waheshimiwa Wabunge,
inakusudia kuweka bayana katika kitabu cha Mpango
utakapokamilika muhtasari wa ushauri uliozingatiwa, na ule
tunaoona unafaa uzingatiwe katika mipango itakayofuata na yale
ambayo bado yanahitaji kuchambuliwa kwa kina kabla ya
kuzingatiwa kwenye mipango.
36. Mheshimiwa Spika, Serikali ya awamu ya Tano imedhamiria
kujenga Tanzania mpya ili kuwaondoa watanzania kwenye lindi la
umaskini haraka. Uamuzi huu unahitaji kuachana na mazoea,
unahitaji sacrifice na unahitaji tufanye kazi kwa bidii, nidhamu na
uadilifu. Tunataka uchumi ambao wananchi wengi wananufaika nao.
Nirudie tena, Serikali ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli
inajali wafanyabiashara lakini budi sheria za nchi zizingatiwe.
37. Mhe. Spika, naomba kutoa hoja.