12

Elimu Ina Umuhimu gani katika Jamii? - HakiElimuhakielimu.org/files/publications/document143wp_07_9_elimu_umuhimu... · Katika mazingira ya kawaida kabisa ndani ya jamii yetu, Imezoeleka

  • Upload
    phamque

  • View
    496

  • Download
    33

Embed Size (px)

Citation preview

Page 1: Elimu Ina Umuhimu gani katika Jamii? - HakiElimuhakielimu.org/files/publications/document143wp_07_9_elimu_umuhimu... · Katika mazingira ya kawaida kabisa ndani ya jamii yetu, Imezoeleka
Page 2: Elimu Ina Umuhimu gani katika Jamii? - HakiElimuhakielimu.org/files/publications/document143wp_07_9_elimu_umuhimu... · Katika mazingira ya kawaida kabisa ndani ya jamii yetu, Imezoeleka

1

Elimu Ina Umuhimu gani katika Jamii?

Kuelekea Elimu Sahihi

Gervas Zombwe1

1. Utangulizi Katika mazingira ya kawaida kabisa ndani ya jamii yetu, Imezoeleka kusikia au kuona watu wakioanisha dhana ya elimu au usomi, maadili, mwenendo au matendo ya mtu. Mathalani, mtu aliyepata elimu kwa kiwango fulani akifanya jambo la ajabu katika jamii inayomzunguka wengi husema; “huyu anafanya mambo ya ajabu kama vile hakusoma.” Wengi wanastaajabu. Hata katika matamshi. Kiongozi mmoja au msomi fulani akitoa matamshi ya hovyo kabisa watu huanza kuhoji usomi wake. Wengi huuliza na kushangaa kwamba, “huyu bwana anasema maneno ya ajabu kama hakusoma.” Kauli kama hizi ni za kawaida kabisa katika jamii yetu na tumezizoea na tunazitumia katika mazingira tunayoishi. Je usomi ni nini? Elimu nini? Mtu aliyeelimika anakuwaje? Elimu ina manufaa gani katika jamii? Malengo ya waraka huu ni kubainisha tafsiri halisi ya elimu kwa kujibu maswali haya na kushabili uhalisia wa mazingira ambamo elimu inafanya kazi. Waraka huu ni mwendelezo wa juhudi za kitaaluma za kukuza uelewa wa nini maana ya elimu, kazi za elimu na malengo ya elimu na umuhimu wa elimu katika jamii, ili jamii iwe na tafsiri sahihi. Kwa maana kwa muda mrefu sasa kumekuwa na upotoshaji wa neno elimu au kumekuwa na uelewa finyu wa maana ya elimu na malengo ya mchakato mzima wa kufundisha na kujifunza. Baadhi ya wazazi na walezi wanaitambua elimu kwa kuangalia uzuri wa shule anayosoma mtoto wao au uwezo wa mtoto kuongea lugha za kigeni kama vile Kiingeza au Kifaransa. Hivyo kwa kuwa na mtazamo kama huu wanatumia juhudi kubwa na rasilimali nyingi kuhakikisha watoto wao wanajua kiingereza tu hata kama hawana maarifa yeyote. Hili ni kundi la kwanza la wanajamii. Kundi la pili ni baadhi ya watawala na watunga sera, wanaojaribu kuitambua elimu kwa kuanngalia nyenzo na vitendea kazi vya shuleni. Kama vile idadi ya madawati, viti na samani za shule kwa ujumla. Aidha kundi hili mara nyingi linachukulia idadi ya watoto madarasni wanapoandikishwa kuwa ndio elimu yenyewe. Na mara nyingi unakuta taarifa zinazotolewa juu ya mchakato wa kujifunza zimejikita katika vitendea kazi tu na sio nini mtoto anapata awapo darasani. Mtazamo wa tatu ni ule wa kuangalia ufanisi wa wanafunzi katika mitihani ya mwisho. Ingawa hili linakaribia ukweli , bado limehamisha kwa kiwango kikubwa maana ya dhana yenyewe. Mtazamo wa kuchukulia kufaulu mitihani kuwa ndio elimu umesababisha mawazo ya wazazi, na hata walimu kutoka kwenye mchakato wa kutoa maarifa hadi mchakato wa kuhakikisha watoto wanafaulu mitihani hata kama hawajui kusoma na kuandika. Nguvu nyingi zinatumika kuwafanya watoto wakariri mitihani iliyopita ili waweze kushinda mithani ya mwisho (Sumra, 2007). Dhamira ya kujenga uelewa na tafsiri moja ya elimu na malengo ya elimu kwa wadau wa elimu, imekuja baada ya mabadiliko ya kasi kimaendeleo yanayochangiwa na utandawazi unaojengwa na

1 Gervas Zombwe ni mchambuzi wa sera, HakiElimu. Barua pepe [email protected] au [email protected]

Page 3: Elimu Ina Umuhimu gani katika Jamii? - HakiElimuhakielimu.org/files/publications/document143wp_07_9_elimu_umuhimu... · Katika mazingira ya kawaida kabisa ndani ya jamii yetu, Imezoeleka

2

nguvu ya maarifa, ubunifu na mwingiliano mkubwa wa tamaduni za jamii mabalimbali. Karibu taarifa za maendeleo za nchi zote ulimwenguni zinakubaliana kuwa elimu ni daraja pekee la maendeleo ya nchi. Kila taifa linahitaji wasomi, linahitaji watu wenye maarifa, ujuzi ubunifu na teknolojia mbalimbali zinazofanya watu kuwa wazalishaji. Bila elimu ni vigumu kwa taifa kupata maendeleo yo yote. . Na kwa sababu malengo ya elimu ulimwengu mzima ni kuleta maendeleo, ni dhahri kwamba, tafsiri sahihi na juhudi madhubuti za kuifikia azma ya kutoa elimu ya kweli kwa kila Mtanzania ni njia mojawapo ya kuharakisha maendeleo katika nchi yetu. Na ndipo tutaweza kuwashinda maaduni watatu aliosema Baba wa Taifa: ujinga, umaskini na maradhi. 2. Maana ya Elimu Wanafalsafa na wanazuoni wa sehemu mbalimbali ulimwenguni, kwa muda mwingi hata kabla ya kuzaliwa kristo wamejaribu kutoa na kufafanua maana ya elimu katika muktadha tofautitofauti. Pamoja na wingi wa fafanuzi hizo za wanafalsafa na wanazauo bado, kuna maeneo wanakutana na kukubaliana. Karibu wote wanaiona elimu kama mchakato, pili wanaiona elimu kama mabadiliko au ujenzi wa binadamu na tatu wanaiona elimu kama maisha ya mtu katika jamii. Sera ya Elimu na mafunzo ya Wizara ya Elimu nchini Tanzania inatoa maana ya elimu kuwa ni mchakato ambapo mtu hupata maarifa na ujuzi wa kujitambua na kujiweka sawa katika kupambana na mazingira na mabadiliko ya mara kwa mara ya kijamii, kisiasa na kiuchumi. Aidha ni njia ya mtu kuweza kuutambua uwezo wake kamili (URT, ETP 1995: v). Kamusi ya Webster, inafafanua elimu kuwa ni mchakato wa kufundisha au kukuza maarifa, stadi na maadili ya wanaojifunza. Elimu ni mchakato wa kuendeleza uelewa na upatikanaji wa maarifa. Uelewa huo ni ule unaofuata muundo wa sera na utekelezaji wa matakwa yaliyowekwa. Elimu hiyo hujidhihirisha kwa mabadiliko yanayotokea ndani ya mtu kufikia mahitaji ya jamii husika (Qorro; 2006). Elimu ni mfumo wa kujifunza na kufundisha unaozaa maarifa rasmi, maarifa matumizi, yaani ujuzi na stadi za maisha, pia maarifa ya upeo wa upembuzi na ubunifu, ambayo kwayo mtu hupata uwezo wa kufanya jambo jipya katika jamii (Senge. 2000 187). Ishumi wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam, katika kitabu chake cha Philosophy of Education anafafanua mitazamo miwili ya elimu, kwanza elimu inaweza kuangaliwa kama kiwango cha mkusanyiko wa ufahamu wa mtu na ubora wa taarifa au uelewa unaomuweka juu ya mtu mwingine kiuwezo2. Pili, elimu ni mchakato wa mwendelezo unaohusisha mtu na vitu vingi kama kupata taarifa, ujuzi na maarifa anayoweza kuyatumia katika mazingira mbali mbali kutatua matatizo na changamoto zinazomsibu (Ishumi & Nyirenda, 2002: 41). Mwalimu Nyerere alifafanua elimu kama mchakato unaomuandaa mtu aweze kukabili mazingira anayoishi. Maana mchakato huo unampatia mtu maarifa, ujuzi, maadili, stadi za maisha na uwezo wa kujitambua na kutambua majukumu yake kwenye jamii; hivyo kuwa mzalishaji na sio nyonyaji (anayejitegemea). Na maarifa, ujuzi na stadi hizi ni mwendelezo ambao hauna kikomo, na hivyo elimu ni mchakato usio na kikomo (Nyerere, 1968). Kwa kutambua hivyo Mwalimu Nyerere aliifanya dira ya elimu ya nchi kuwa elimu ya kujitegema. Kwamba elimu inapaswa kuwa mwanga wa ustawi wa jamii nzima, ichochee ushirikiano, haki na usawa katika jamii. Pia ilenge kwenye uhalisia wa maisha ya Tanzania. 2 Nyirenda & Ishumi (2002) Philosophy of Education, Conceptualising the Education Process pg 40

Page 4: Elimu Ina Umuhimu gani katika Jamii? - HakiElimuhakielimu.org/files/publications/document143wp_07_9_elimu_umuhimu... · Katika mazingira ya kawaida kabisa ndani ya jamii yetu, Imezoeleka

3

Hivyo Mwalimu akapendekeza mambo yafuatayo: kuleta mabadiliko ya maisha ya watu vijijni, walimu na wanafunzi wanapaswa kushirikiana katika shughuli za uzalishaji, na wanafunzi washiriki katika maamuzi ya kuzipangilia shughuli hizo ili wajifunze na wajue. Kazi za uzalishaji ziingizwe pia kwenye mitaala rasmi shuleni ili wanafunzi wapate stadi kamili za kazi na kujua na kuthamini kazi kwa kupata nadharia darasani na vitendo nje ya darasa. Hii ingewafanya kuwa wataalamu na wazalishaji pindi wamalizapo masomo. Mitihani ishushwe daraja na kwamba kumjenga mtu iwe kipaumbele badala ya kufaulu mitihani3 tu. Watoto waanze shule wakiwa na umri wa miaka 7 ili wawe na uwezo wa kujitegemea na kujiingiza katika shughuli za uzalishaji mara wamalizapo elimu ya msingi. Na mwisho, elimu ya kujitegema iundwe na stadi zinazojitosheleza, hata elimu ya msingi ijitosheleze na kumwezesha wanafunzi kuishi pindi amalizapo, isiwe kama daraja tu la kupitia kuelekea elimu ya juu. Wanafunzi ni lazima wawe watu wenye kufikiri, wenye kuthamini kazi, wanaojitambua na wenye kujiamini, wanaoshirikiana na wenye upeo wa kubuni na kujifunza zaidi, hawa ndio watakaoiongoza jamii kwenye maendeleo ya kweli.4 3. Malengo ya Elimu Malengo ya elimu na mafunzo hapa Tanzania yamebainishwa na Sera ya Elimu na Mafunzo ambayo ndio sera mama ya mfumo wa elimu hapa nchini. Sera hiyo inabainisha malengo ya elimu kwa ujumla kuwa ni “kuelekeza na kukuza maendeleo na kuboresha haiba ya wananchi wa Tanzania, rasilimli zao na matumizi bora ya rasilimali hizo katika kuleta maendeleo ya mtu binafsi na ya taifa. Kuboresha utambuzi na uhifadhi wa utamaduni, mila na desturi za watu wa Tanzania. Kukuza kujifunza na matumizi bora ya kujua kusoma, kuandika na kuhesabu, maarifa na stadi za kijamii, kisayansi, kifundi, kiteknolojia, kiutaalamu na kwa aina nyingine ya ujuzi. Stadi na uelewa katika maendeleo na uboreshaji wa hali ya mtu na jamii. Kuendeleza na kukuza, kujiamini na kuwa na moyo wa kujiamini, kudadisi, weledi na heshima kwa utu na haki za binadamu na kuwa tayari kufanya kazi kwa kujiendeleza na kwa maendeleo ya taifa. Kuwezesha na kupanua upeo wa kupata, kuboreshana kukuza stadi za maisha za kiakili, kivitendo, za uzalishaji na nyinginezo zitakiwazo katika kutosheleza mahitaji yanayobadilikabadilika mara kwa mara kwa viwanda na kiuchumi. Kumwezesha kila raia kuelewa misingi ya katiba ya taifa pamoja na haki za binadamu na uraia, wajibu na majukumu yanayoendana nayo. Kukuza utashi wa kuheshimu kazi za kujiajiri na kuajiriwa na kuboresha mwenendo katika sekta za uzalishaji na huduma. Kujenga misingi ya maadili ya kitaifa na yanayokubalika,ushirikiano wa kitaifa na kimataifa, amani na sheria kwa njia ya kujifunza, kuelewa na kuzingatia vipengele vya katiba ya taifa na matamko mengine ya msingi ya kitaifa’’.5 Mwaka 2005, Serikali ya Tanzania ilitoa mitaala mipya na kuandika miongozo au silabasi. Katika mitaala na miongozo hiyo malengo ya elimu yamebainishwa wazi. Kwa mfano malengo ya elimu ya msingi peke yake yako 18 kama ifuatavyo; “Kupata stadi za Kusoma, Kuandika, Kuhesabu, ubunifu na kuwasiliana kwa luhga ya Kiswahili, Kiingereza na nyingine za kigeni. Kujenga ari ya kuendelea Kujifunza. Kujenga uwezo wa kufikiri kiyakinifu na kufanya maamuzi yenye mantiki. Kutatua matatizo, kwa kuwa mbunifu na kutumia mikono kuunda vitu anuai. Kutambua kuheshimu na kupenda kufaanya kazi. Kujenga tabia, mwenendo na maadili yanayokubalika katika jamii. Kutambua jinsi matukio ya zamani yanavyoathiri matukioa ya sasa na ya siku zijazo. Kujielewa na kuheshimu utu wake, nafsi yake, utashi wake na nafasi yake katika jamii, kujenga na kuthamini nidhamu binafsi na usawa wa kijinsia.

3 Kauli ya Nyerere aliyoisisitiza sana katika uhai wake hasa ndani ya kitabu chake binadamu na Maendeleo 4 Nyerere, J. (1968) Freedom and Socialism. A Selection from Writings & Speeches, 1965-1967 5 Wizara ya Elimu na Utamaduni Sera ya elimu na Mafunzo 1995 ukurasa wa 1

Page 5: Elimu Ina Umuhimu gani katika Jamii? - HakiElimuhakielimu.org/files/publications/document143wp_07_9_elimu_umuhimu... · Katika mazingira ya kawaida kabisa ndani ya jamii yetu, Imezoeleka

4

Kuielewa na kuitunza afya yake ya watu wengine. Kuelewa, kuthamini na kutumia lugha ya Kiswahili kwa ufasaha. Kupenda na kuthamini utamaduni wa Kitanzania na utamaduni uliobora wa jamii nyingine nje ya nchi. Kutambua na kuthamini Mataifa mengine na jamii zake. Kujenga moyo wa uzalendo na upendo kwa taifa lake na kutathimini uhusianao wa amani. Kukuza uwezo binafsi wa kiakili. Kujenga ari ya kutimiza wajibu katika jamii na kutumia vyema muda wa mapumziko na kutambua, kutumia teknolojia na kuthamini mchango wake katika maendeleo ya taifa na kimataifa’’. 4. Uhusianao kati ya Elimu na Maendeleo Jamii kubwa inahusisha elimu na maendeleo ya watu; ni ukweli ulio wazi kwamba vitu hivi viwili havitenganishwi. Sera ya Elimu na Mafunzo pia imebainisha uhusianao huu kwa kina. Kwamba; “Uhusianao baina ya elimu na maendeleo hutegemea kiasi gani aina ya elimu itolewayo na njia zitumikazo zinaweza kukidhi matazamio ya mtu binafsi na matakwa ya jamii. Falsafa elekezi ya jitihada zote za maendeleo nchini Tanzania ni kufananisha kujitegemea??. Hivi sasa malengo ya jumla ya shughuli za kijamii, kiuchumi na kisiasa yataendelea kuwa ni binadamu, yaani wananchi wote wa Tanzania bila kujali rangi, jinsia au hali zao zingine za asili. Hii inamaanisha kwamba kwa maendeleo ya Tanzania, watu wataendelea kujitegemea zaidi wao wenyewe na rasilimali zao pamoja na jitihada zao wenyewe, yaani ardhi, nguvu zao na utayari wao wa kufanya kazi kwa bidii. Kwahiyo Tanzania inawania na imejitoa kuendelea kutafuta maendeleo yanayamweka mtu kuwa ndiyo kitovu cha maendeleo hayo na katika kufanya hivyo, hujali zaidi maendeleo ya usawa na endelevu kwa siku za usoni, ili binadamu aweze kuishi kwa amani, umoja, uelewanona ushirikiano. Sharti kuwepo na kutoshelezwa kwa mahitaji ya msingi ya chakula, malazi, maji safi na salama, mazingira bora pamoja na maendeleo yenye ufanisi katika kilimo na viwanda. Watu wanategemea kunufaika kutokana na uzalishaji wa mifugo bora, uvunaji sahihi na bora wa maliasili, upanuzi wa viwanda na ubora wa viwango vya mazao ya viwanda. Hatua hizi muhimu zinatamkwa katika upanuzi na uboreshaji zaidi wa biashara, matumizi ya vyanzo vingine vya nishati ambavyo vinaweza kudumisha ufanisi katika uchukuzi na mawasilianao, usimamizi bora zaidi na utunzaji wa mazingira. Upanuzi wa fursa za kujiajiri na ajira za kulipwa utakuwa ndio tumaini kuu kwa vijana. Hali kadhalika, huduma za jamii zilizoboreshwa na zinazofanya kazi, kama vile upatikanaji wa maji safi na salama, afya na elimu zitakuwa ndizo tegemeo la kila mwananchi. Lakini kwenye jamii inayohitaji maendeleo, malengo ya elimu yaliyowekwa yanaweza yasifikiwe kwa urahisi bila sera ya jumla iliyo kamilifu ya kutekeleza mipango na shughuli zote za maendeleo (URT, ETP 1995, xi). 5. Kazi za elimu katika jamii Kazi za elimu ni matokeo au mazao yanayozaliwa kutokana na maarifa. Mchakato wa kujifunza unampa mtu maarifa anakuwa msomi. Jinsi anavyoyatumia maarifa hayo katika ulimwengu wa kazi kwa kufanya kazi au kubuni kitu ndipo tunapata mazao au matunda ya usomi. Haya hujidhihirisha kwa wasomi au watu waliopata elimu. Kutokana na maarifa na ujuzi, wanapata uwezo wa kufanya mambo mengi mapya kwa usahihi, na ubunifu mkubwa unajengeka ndani mwao. Na hivyo kuwafanya wawe watu muhimu katika kuwaongoza wenzao kwenye maendeleo

Page 6: Elimu Ina Umuhimu gani katika Jamii? - HakiElimuhakielimu.org/files/publications/document143wp_07_9_elimu_umuhimu... · Katika mazingira ya kawaida kabisa ndani ya jamii yetu, Imezoeleka

5

ya kweli. Tunamoishi matendo ya wasomi, kazi za wasomi, majukumu ya wasomi na shughuli mbali mbali zinazofanywa na watu waliopata elimu ndizo zinadhirisha kazi ya elimu katika jamii. Zao la kwanza muhimu sana la elimu ni kuwa na uwezo mkubwa wa kufikiri kwa makini na kiyakinifu. Uwezo huu ndio unaohitajika sana katika jamii ya leo. Mtu mwenye uwezo wa kufikiri ndio mwenye nguvu ya kuibua dhana mpya, kutafuta njia mbadala za kutatua matatizo na kuelekeza wenzake katika matendo sahihi. Uwezo wa kufikiri ndio unaomwongoza mtu kila siku katika utendaji wake. Mathalani, mtu anayekabiliwa na changamoto au tatizo lolote, kabla ya kulitatua ni lazima afikirie kwanza, akishafikiria ndipo anapanga njia mbadala na kuziweka kwenye matendo na tatizo linatatuliwa. Kufikiri kupita mipaka tuliyoizoe ndiko huleta maendeleo makubwa na ya haraka. Watu walioibua teknolojia hizi tuzionazo, waliongozwa kwanza na upeo wa kufikiri kiundani ndipo wakaibuka na dhana mpya. Kwa mfano, huwezi kupata wazo la kutengeneza gari bila kufikiri kiundani na kuvuka mipaka ya dhana hiyo. Au waliotengeneza ndege na kubuni dhana mpya pamoja na vifaa vingi vya kisasa tunavyotumia kila siku walianza na wazo kwanza lililofikiriwa kwa undani mno. Hakuna mafanikio yeyote duniani yanayoweza kupatikana bila kutanguliwa na fikra yakinifu zinazovuka mipaka tuliyozoea kufikiri. Tendo la kufikiri ni la kila siku na la ndani ya akili na utashi. Kazi yeyote inayofanyika kwa kutanguliwa na kufikiri huzaa matunda na huwa halisi, bila kufikiri kwanza matokeo ya juhudi za mtu mara nyingi huwa ni anguko au hasara. Ndiyo maana katika mazingira ya kawaida. Mtu akifikiri na kuibua jambo jipya lenye manufaa imezoeleka kusikai watu wakihoji”hivi ulifikiri nini hadi ukafanya hivi” au ulipata wapi wazo na kuandika kitu hiki cha ajabu? Mshangao huu bado ulimwengu mzima unaendelea kushanaga kuhusu wanafalsafa wa mwanzo waliofikiri vitu vingi na kanuni nyingi zilizokuja kutumiwa na wanasayansi na wajuzi kuunda vitu kama magari na ndege. Mfano mzuri ni mawazo ya Issack Newton, na wanafalsafa akina Socrate, Plato Galileo Galilei, Mwalimu Nyerere na wengine wengi. Nguvu ya kufikiri ndiyo hubadilisha dunia. Kazi za elimu pia zinajidhihirisha katika uwezo wa watu kubuni njia mbadala za kutatua matatizo yao. Ubunifu ni uwezo wa kuleta na kutengeneza njia mbadala za kufanya jambo, au kutengeneza fursa mpya iliyo bora zaidi. Taarifa nyingi za kimataifa na kitaifa zinabaini kwamba dunia ya leo ni ya wabunifu. Ulimwengu wa sayansi na teknoljia unaundwa na wabunifu. Katika jamii watu waliosoma wanatarajiwa kuwaongoza wenzao wasiosoma au wenye maarifa kidogo katika kubuni njia mbadala za kujiendeleza kama vile kubuni fursa kwa kutengeneza miradi, kubuni biashara mbambali, kuanzisha viwanda, kubuni dhana mpya zinazoelekeza kwenye mafanikio, kubuni njia nyingi za kutangaza biashara. Mfano mzuri ni makampuni mengi ya simu za mkononi, kila siku yanabuni njia mpya za kuvutia wateja kwa kutoa matangazo ya kuvutia. Ubunifu una uwanja mpana na wigo usiozibika. Wapo wabunifu wa akili wanaoibua dhana mpya kila siku zinazotumiwa na watu kujiendeleza. Wapo wabunifu wa kuunda vitu kwa mitindo mbalimbali, wapo wabunifu wa mahusiano katika jamii na mwingiliano wa watu, na wapo wabunifu wa kuvumbua vitu mbalimbali. Hawa wote ni muhimu katika ulimwengu huu wa sayansi na teknolojia ambamo maarifa mapya yanaibuka kila leo na ushindani wa kibiashara unapanuka kila siku. Kazi ya elimu ni kujenga watu wanaojitambua na kujithamini. Kujitambua ni jambo la msingi sana katika maisha. Kujitambua huko kunaendana na uwezo wa mtu kujua yeye ni nani anawajibu gani katika jamii. Anapaswa kufanya nini kwa manufaa yake, familia na jamii kwa ujumla. Mtu akijitambua atakuwa na uwezo wa kufanya mambo yanayokubalika katika jamii. Kwa mfano, atawajibika ipasavyo kuanzia nyumbani hadi ofisini. Atatii sheria za nchi, atatawala maumbile yake, atakuwa mzalishaji katika jamii yake, atatumia haki yake kama raia mahali popote aendapo

Page 7: Elimu Ina Umuhimu gani katika Jamii? - HakiElimuhakielimu.org/files/publications/document143wp_07_9_elimu_umuhimu... · Katika mazingira ya kawaida kabisa ndani ya jamii yetu, Imezoeleka

6

kama vile kupiga kura. Kuchangia maendeleo kulipa kodi, na kuthamini kazi. Kinyume chake, mtu asiyejitambua ni sawa na gari linalosafiri usiku bila taa. Elimu ni lazima iwape watu uwezo wa kuchambua taarifa zilizopo na kubashiri matokeo ya wakati ujao ili kufanya maamuzi sahihi. Ujuzi wa kufanya maamuzi sahihi katika maisha unakuja tu pale mtu anapokuwa na uwezo wa kuchambua taarifa kiyajinifu na kubashiri nini kitatokea baadaye maamuzi fulani yatakayochukuliwa. Mathalani, kuna kampeni zinazoendelea za kupambana na UKIMWI na madawa ya kulevya, kampeni hizi zinabeba ujumbe “fanya uamuzi sahihi au timiza matarajio yako.” Hii inamaanisha kuwa watu wanauwezo wa kuzuia ukimwi iwapo watachambua taarifa za ukimwi na kujua matokeo ya ukimwi. Hii inanfanya mtu aache ngono zembe na kujilinda yeye na familia yakeo. Lakini pia tuna mifano mingi mizuri katika jamii imezoeleka kusikika watu wakisema, “kubali ushauri lakini usikubali maamuzi”. hii inamaanisha kwamba mtu anapaswa kuchambua taarifa anazopewa (ushauri) kisha kubaini matokeo yajayo kama ni mema au mabaya, ndipo anachukua uamuzi fulani. Iwapo mtu atashauriwa kuiba na yeye akakubali watu watasema huwa ana washauri wabaya, maana yake mwishoni matokeo ya wizi ni mabaya. Nguvu ya kutoa maamuzi sahihi ni msingi wa maendeleo ya nchi yeyote. Wasomi wanaopata elimu hata ya msingi tu inatosha sana kuwapa uwezo wa kufanya maamuzi sahihi. Mtoto mdogo anapokua kati ya miaka miwili hadi 3 anaweza kuambiwa na mzazi wake “shika moto” naye akashika bila kujau madhara yake, kwa maana hana uwezo wa kuchambua hiyo taarifa na kutabiri matokea yake. Lakini mtoto huyo huyo akifikia umri wa mika 4 na kuendelea ukimwambia jambo hilo, hawezi kulifanya; Kwa maana tayari anauwezo wa kuchambua taarifa na kujau matokeo yajayo kutokana na taarifa hiyo. Mfano huu ni halisi na dhahiri katika maisha yetu ya kila siku. Kwahiyo uwezo wa kuamua kwa wasomi au watu wanaopata elimu unapaswa kuwa mkubwa zaidi na hasa kwenye mambo nyeti ya maendeleo na maisha kwa ujumla. Maamuzi yeyote yanayofanywa na wasomi yanayoliangamiza taifa ni usaliti wa wasomi hao kwa wanajamii waliowategemea. Mtu aliyesoma anauwezo mkubwa wa kufanya maamuzi sahihi kwa sababu anaweza kutabiri matokeo ya maamuzi na kuchambua taarifa sawasawa. Kazi ya elimu pia ni kukuza uwezo wa kutatua matatizo kwa wanajamii. Uwezo wa kutatua matatizo unatokana na uwezo wa kutafuta njia mbadala na kutathimini kivitendo. Bila kutafuta njia mbadala ni vigumu kutatua matatizo. Kwa mfano, tatizo la malaria katika familia, ni rahisi msomii kutumia maarifa yake kwa utambuzi kwamba usafi wa mazingira yanayozunguka nyumbani njia mbadala ya kutatua tatizo pia kupulizia dawa na kuweka vyandarua ni njia mbadala. Tatizo la mmonyoko wa udongo mtu anaweza kutatua kwa kwa kupanda miti na kuweka matuta ya mkingamo. Hata watoto wadogo tatizo la kuchomwa miiba hasa huko vijijini kila mara waendapo shule, mtoto anafikiri kuanza kuvaa viatu au kusafisha njia anayopita kwenda shule na hapo tatizo linakwisha. Uwezo wa kutatua matatizo una ambatana na fikra yakinifu na upeo wa kuona mbali. Kila siku katika changamoto huibuka maisha. Chamgamoto hizo zinahitaji utatuzi, ndipo mtu anapaswa kuwaza na kufiria mbinu za suluhisho ya matatizo yanayomkabili. Elimu ina kazi kubwa ya kujenga watu wenye maadili mema na wenye mwenendo unaokubalika kwenye jamii. Maadili ni kitu cha msingi sana kati jamii. Bila maadili jamii haiwezi kuwa ya kistaarabu hata siku moja. Kwa mfano, msomi hata wa elimu ya msingi tu anatarajiwa awe na maadili yanayokubalika katika jamii anayoishi. Kama vile umoja, upendo mshikamano, kushirikiana katika kazi, tabia njema, kuthamini kazi na kufanya kazi kwa bidii. Mathalani tatizo la rushwa hapa Tanzania linahusishwa na kukosekana kwa maadili kwa baadhi ya viongozi na wanajamii wanaokula rushwa. Mtu mwenye maadili hawezi kukosa upendo wa

Page 8: Elimu Ina Umuhimu gani katika Jamii? - HakiElimuhakielimu.org/files/publications/document143wp_07_9_elimu_umuhimu... · Katika mazingira ya kawaida kabisa ndani ya jamii yetu, Imezoeleka

7

kumhudumia mgonjwa na kumwacha anakufa eti kwa sababu hajatoa sh 5000 ya hongo. Mtu mwenye maadili ya kuthamini utu na wanajamii wenzake hawezi kuwaibia wananchi mabilioni ya pesa na kuyaweka benki za nje na kuwaacha Watanzania wenzake wanakufa kwa njaa. Mtu wa namna hii tunasema hana maadili na elimu aliyopata haikumsaidia. Labda ni elimu ya cheti tu. Maadili ndiyo yanaongoza jamii, iwe maofisini kuna maadili ya kazi, na hata kwenye taasisi binafsi na za dini kuna maadili ambayo kila mmoja anapaswa kufuata. Mwenendo na matendo ya mtu hudhihirisha usomi wake na kiwango cha maadili alichonacho. Elimu inatarajiwa kuzalisha watu wanaopenda kazi na kuthamini kazi.6 Watu wanajishughulisha na kazi za aina mbalimbali ili kujipatia kipato. Tena kazi hizo zitafanywa kwa ubunifu mkubwa na hivyo mazao yatakuwa na tija kubwa. Mathalani, watu wapende kilimo kama wako kwenye mazingira ya kulima ili wazalishe chakula kingi kwa ajili yao na jamii nyingine. Watu wafuge mifugo kwa njia za kisasa na kupata mapato mengi. Kukaa bila kazi na uvivu wa kupenda mapato bila kazi ni ushahidi kwamba elimu uliyopata ni ya cheti haikusaidia lolote. Hata kama ni ajira za ofisini ndani ya ofisi kuna kazi nyingi tena za kutumia maarifa ya hali ya juu. Kukaa ofisini bila kufanya kazi sio tafsiri ya elimu. Huo ni utwana! Elimu izalishe watu wanaotengeneza ajira na watu walioajiriwa katika sekta mbalimbali. Kuwa wataalamu na taaluma za kila namna ambazo watu wake wanapaswa kufanya ili kujiletea maendeleo. Mathalani, katika jamii tunao madakatari nao wanauwezo wa kufanya kazi za utabibu vizuri, wapo walimu wanaojenga watoto wetu kwa kuwapatia maarifa, kuamsha na kuchochea hisia za kujifunza. Wapo wahandisi wanaongoza mitambo na ujenzi wa miundo mbinu mbali mbali. Wapo wahasibu na wanauchumi wanatafsiri namba (tarakimu) kwenda kwenye uhalisia na kuona mwelekeo wa mapato na uchumi wetu. Haya ndio mazao ya elimu. Nchi bila kuwa na elimu inayozalisha watu wenye uwezo, kamwe haiwezi kupata maendeleo. Elimu inawapa wanajamii stadi za mawasiliano na kujiamini ili wawasiliane kwa usahihi na kwa manufaa. Stadi za mawasiliano ndizo msingi wa upashanaji habari. Yaani, uwezo wa kujua kuandika kusoma, kuhesabu, kujieleza na kutoa maoni katika jamii. Msomi yeyote anapaswa kuwa na ujasiri wa kujieleza, kudadisi na kuhoji mienendo isiyoenda sawa. Aidha kuhoji na kudadisi kunapaswa kuambatana na mibadala ya suluhu za matatizo. Watu wasio an uwezo wa kuhoji, kujieleza na kutumia haki ya kupata habari na kutoa habari ni mazao ya elimu dhaifu. Kuanzia elimu ya msingi hadi chuo kikuu kwa hatua mbalimbali kulingana na ngazi mtoto anapaswa kuwa na stadi hizi muhmu. Sio kuwa mtu wa kukubali kila kitu, kuona kila kitu na kunyamza, na kujivika ububu bandia. Jamii inamhitaji msomi aiongoze kweye nuru ya maendeleo kupitia michango ya mawazo katika mijadala, makongamano, katika familia na kwenye jamii kwa ujumla. Msomi aisiyefanya hivi anakuwa msaliti kwa jamii iliyomsomesha na kwa taifa zima. (Mandera: 1981) 6. Ushirikiano katika kutoa elimu sahihi Kutokana na ukweli kwamba mchakato mzima wa kujifunza na kupata elimu unalenga jamii, kwa manufaa ya jamii, ni jambo la msingi kuwa na ushirikiano katika kufikia malengo ya utoaji elimu. Mchakatao hu unagusa kila mmoja kwa nafasi yake. 6.1 Wazazi Hawa ni watu wa kwanza katika mchakato huu wakutoa elimu. Mwalimu Nyerere alishawahi kuwaweka wazazi na walimu kuwa ni watu wa kwanza katika mchakato. Nanukuu…“Wale wenye wajibu wa kufanya kazi na vijana wa umri mdogo wana nguvu kubwa zisizozidiwa na nguvu za 6 Nyerere, 1967 Makala za ujamaa na kujitegema katika Tanzania huru

Page 9: Elimu Ina Umuhimu gani katika Jamii? - HakiElimuhakielimu.org/files/publications/document143wp_07_9_elimu_umuhimu... · Katika mazingira ya kawaida kabisa ndani ya jamii yetu, Imezoeleka

8

yeyote yule kwa kutilia maanani hali ya baadaye ya jamii, Nguvu hizi zipo katika makundi mawili-wazazi na Walimu.’’7 Wazazi wanajukumu la kuwalea watoto wao katika misingi bora ya maadili yanayowajega kuwa tayari kujifunza na kupokea maarifa. Shule ya kwanza ya mtoto ni mzazi maana ndiye anayekaa na mtoto tangu akiwa mdogo. Mabali na maadili mzazi anawajibu wa kumtia moyo mtoto na kufuatilia mchakato wa kujifunza wa mtoto. Pia kumpatia mtoto mahitaji ya kusomea kama vile vifa vya kujifunzia nyumbani, madaftari ya shule sare za shule na hata michango ya shule. Kujua shauku za mtoto na kujua matatizo anayoyapata katika kujifunza kwake. Kumjengea mtoto fikra za kujifunza kwa kumuonesha mifano halisi ya uzuri wa kujifunza ili aone shule ni mahali pazuri na pa manufaa kwake. Mtoto akilelewa katika mtindo huu atakuwa na hamu ya kujifunza mara zote na atakuwa tayari kujifunza na kufundishwa. 6.2 Walimu Ndio hasa watekelezaji wa mchakato mzima wa kutoa elimu. Mwalimu ndio dira ya mwelekeo wa mwanafunzi. Mwalimu anauwezo mkubwa wa kumfanya mtu aliyekuwa anaelekea kuwa daktari akawa jambazi! Pia mwalimu anauwezo wa kumrudisha kijana aliyekuwa anataka kupotea katika makundi ya wavuta bangi na machangudoa, na kuwa daktari bingwa wa kutegemewa. Ukweli huu aliujua sana Mwalimu Nyerere. Walimu ndio wanachagiza ari ya kujifunza na kuamsha hisia na mihemko ya wanafunzi. Ndio wanatoa maarifa na kuamsha hisia za ubunifu kwa wanafunzi pamoja na kujenga ari ya kujifunza kwa mwanafunzi siku zote. Walimu ndio wanaojua na kusimamia tabia na mwenendo wa wananfunzi kila siku kulingana na makuzi yao. Hivyo walimu wenye moyo, taaluma na utaalamu wa kufundisha ndio daraja la maendeleo ya mwanafunzi. Bila kuwa na walimu bora na wenye moyo ni ngumu mno kufikia malengo ya elimu na matunda ya elimu kamwe hayatabainika katika jamii. 6.3 Mitaala Ni muhimu kuwa na mitaala inayoshabihiana na mahitaji halisi ya jamii. Mitaala au miongozo isiyofaa ni kikwazo cha utoaji maarifa. Mwalimu Nyerere siku zote alisisitiza uhusiano wa elimu na maisha. Alipata kuitaja elimu kama mkombozi8 akimaanisha kwamba elimu ni lazima imkombe mtu kwa kumpa maarifa na uwezo wa kuzikabili changamoto katika mazingira anayoishi. Hivyo mitaala inapaswa kutungwa kulingana na mahitaji yetu. Ikiwaelekeza walimu kufundisha kile kinachohitajika kwenye jamii yetu. Mathalani, mitaala inamtaka mwalimu afundishe miyeyuko ya Barafu huko ulaya mashariki au Asia, hii haitamsaidia mtoto wa msukuma au mmasai anayetaka kujua mbinu za ufugaji bora na kilimo bora. Kwa hiyo mitaala kama hii hailingani na mahitaji yetu kwani hatuna barafu zinazoyeyuka katika jamii. Hivyo uandaaji wa mitaala na miongozo ni jambo la msingi kufikia elimu inayohitajika katika jamii husika. Bila kuwa na mitaala inayoshabihiana na mahitaji yetu tutakuwa na wasomi wasio na manaufaa kwa jamaii husika. Mtu aliyesoma na kubobea katika jiografia ya miyeyuko ya barafu utaalamu wake hauna faida ya moja kwa moja katika jamii isiyo na barafu. 6.4. Dira na Sera sahihi Mfumo wowote wa utoaji elimu katika jamii unapaswa kuongozwa na mwelekeo sahihi wa kufikia malengo yanayojulikana, yaani dira ya elimu. Dira ndiyo inayoongoza mchakato mzima wa kujifunza na kufundisha maana kila mmoja atapita katika njia sahihi kuelekea lengo kusudiwa la taifa. Enzi za Mwalimu Nyerere dira ya elimu ya Tanzania ilikuwa ni kutoa elimu ya kujitegemea. Hivyo, michakato yote ya elimu enzi hizo ililenga kufikia lengo hilo la kumfanya mwanafunzi apate maarifa stadi na uwezo wa kuzalisha kisha ajitegemee mwenyewe katika kuishi. Kweli, wanafunzi kuanzia ngazi ya elimu ya msingi tu waliweza kuzalisha na kuishi vijijini na

7 Maneno ya Mwalimu Nyerere katika Hotuba yake ya Agosti 27 1966 8 Nyerere 1967, Education for self reliance

Page 10: Elimu Ina Umuhimu gani katika Jamii? - HakiElimuhakielimu.org/files/publications/document143wp_07_9_elimu_umuhimu... · Katika mazingira ya kawaida kabisa ndani ya jamii yetu, Imezoeleka

9

mijini bila taabu maana walikuwa na stadi za maisha na maarifa ya kuishi. Je dira ya elimu ya leo ni nini? Hili swali watu wengi wanajiuliza. Kukosa dira ni sawa gari linalokwenda bila dereva, haliwezi kufika maana halijui linakokwenda. Inawezekana hata katika mfumo wetu wa sasa wa elimu usio na dira sahihi ndio umezaa tatizo la utoaji elimu kiholela kila mtu na malengo yake. Wengine wanajitahidi kutafuta vyeti tu, wengine kutafuta kufaulu mtihani tu, wengine wanajitahidi kupata takwimu za uandikishaji tu, na wengine wanajitahidi kuwafunza watoto kiingereza tu. Hawa wote wanajiita wanatoa elimu. Je kwa tofauti hizi maendeleo yatafikiwa kweli? Serikali ni mdau mkubwa wa elimu. Na mchango wake katika kuhakikisha elimu inakwenda mbele ni mkubwa. Kwanza, kwa kuweka dira sahihi ya elimu, kuweka sera nzuri zinazotekelezeka, kusomesha na kuajiri walimu wa kutosha na wenye sifa, kupeleka vifaa vya kufundishia na kujifunzia shuleni na vyuoni na kusisimamia kikamilifu utekelezaji wa mipango ya elimu. Kwa kufanya hivyo ndipo elimu sahihi itaweza kutolewa. Vingineyo ni vigumu kukuta elimu sahihi au bora bila serikali kuwajibika sawasawa. 7. Hitimisho Nihitimishe kwa kunukuu tena kauli za Mwalimu Nyerere, kwamba, “kwa watu masikini kama sisi elimu inafaa kuwa chombo cha ukombozi.’’ Usemi huu bado ni hai na ndio ukweli wenyewe. Mtu anayepata maarifa ndio anayekuwa na uwezo wa kuzikabili changamoto katika mazingira yake. Mwalimu aliwahi kusema pia “…ukitaka kumsaidia mtu maskini somesha watoto wake.’’ Hapa ujumbe ni uleule thamani ya elimu katika kumkomboa mtu. Na mwisho Mwalimu aliifafanua elimu kuwa.. “elimu inatakiwa kuwaandaa vijana wetu kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa taifa…ambamo mabadiliko ya maendeleo yanapimwa kwa kuzingatia ubora wa maisha ya mtu na siyo majengo ya kifahari, magari, au vitu vingine vya aina hiyo’’ (Nyerere1922-1999).

Page 11: Elimu Ina Umuhimu gani katika Jamii? - HakiElimuhakielimu.org/files/publications/document143wp_07_9_elimu_umuhimu... · Katika mazingira ya kawaida kabisa ndani ya jamii yetu, Imezoeleka

10

Marejeo Nyerere, J. (1968). Freedom and Socialism. A Selection from Writings & Speeches, 1965-1967, Dar es

Salaam: Oxford University Press. This book includes The Arusha Declaration; Education for self-reliance; The varied paths to socialism; The purpose is man; and socialism and development.

Nyerere, J. (1974). Freedom & Development, Uhuru Na Maendeleo, Dar es Salaam: Oxford University Press. Includes essays on adult education; freedom and development; relevance; and ten years after independence.

Nyerere, J. (1977). Ujamaa-Essays on Socialism, London: Oxford University Press. Nyerere, J. (1979). Crusade for Liberation, Dar es Salaam: Oxford University Press. Nyerere, J. (1978). "Development is for Man, by Man, and of Man": The Declaration of Dar es

Salaam' in B. Hall and J. R. Kidd (eds.) Adult Learning: A design for action, Oxford: Pergamon Press.

Nyirenda, S. D. & Ishumi G. M. (2002). Philosophy of Education.An Introducation to concepts, Principles and Practice. Dar-es-Salaam: Dar es salaam University press

Qorro M(2006). Does language of Instruction Affect Quality of Education. HakiElimu working paper serie 8.

Senge, J. (2000). Schools that Learn, New York: DoubleDay Publishing Group.

Page 12: Elimu Ina Umuhimu gani katika Jamii? - HakiElimuhakielimu.org/files/publications/document143wp_07_9_elimu_umuhimu... · Katika mazingira ya kawaida kabisa ndani ya jamii yetu, Imezoeleka